Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo. Mwezi 4 Rajab ambamo mmoja katika maimamu wetu wane, Imam Shafi-'I aliiaga dunia.
Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad ﷺ, aya hapo juu ya 36 ya Sura Tawbah, inazungumzia utukufu wa miezi minne. Mwezi Rajab, ambao ni mmojawapo kati ya miezi hiyo minne, mwezi ambao una fadhila tele. Ni mwezi ambamo dua hukubalika.
TAFSIRI: Bila shaka idadi ya miezi kwa Allah ni miezi kumi na mbili katika kitabu cha Allah tangu Alipoumba mbingu na ardhi, miongoni mwao minne ni yenye huruma (tukufu). Hii ni dini iliyonyooka na hivyo msidhulumu nafsi zenu katika miezi hizo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wanavyopigana nanyi nyote, na jueni kuwa Allah yu pamoja na wachamungu.
IMAM SHAFI-'I RAHIMAHULLAH.
Jina la Imam Shafi-'I ni Muhammad bin Idris bin Abbas bin Uthman bin Shafi-'I bin Saib bin Ubeid bin Abdi Yazid bin Hashim bin Abdul Muttalib bin Abdi Manaf.
Abdi Manaf ni katika ukoo wa nne wa Mababu zake Mtume ﷺ. Ukoo wa Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam uko hivi: (Sayyidina) Muhammad bin Abdullah bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdi Manaf. Hivyo Mtume ﷺ amezaliwa kupitia mwanae Abdi Manaf (Hashim) wakati Imam Shafi-'I amezaliwa kupitia Abdul Muttalib.
Imam Shafi-'I amekuwa maarufu kwa jina hilo (Shafi-'i) kupitia kwa babu yake katika ukoo wa tatu (Shafi-'i).
Wazazi wake wanatokana na kabila maarufu la kiarabu la Bani Hashim. Baadhi ya sababu ya yeye kuwa na kipaji hicho ni kuwa alikuwa : Imam (kiongozi – wa Dini), Mwanasheria (wa masuala ya sharia za Dini), Mcha Mungu na mtu mwenye hekima na busara. Alikuwa mwandishi wa vitabu vikubwa 14 vya kanuni na falsafa vya sharia ya Kiislam na pia vitabu vingine vidogo zaidi ya 100.
Kila alipopatwa na tatizo, Imam Shaifi-'I alielekea Baghdad kudhuru kaburi la Imam Abu Hanifa, kisha husali rakaa 2 na kumuomba Allah kupitia (wasila) kwa Imam Abu Hanifa. Imam Shafi-'I mwenyewe amesema kuwa hakika maombi yanakubalika katika kaburi la Imam Abu Hanifa.
Imam Shafi-'I alikuwa mwanafunzi wa Imam Malik Radwiy-Allahu Anhu. Alikuwa akihitimisha Quran (Msahafu) nzima katika usiki moja tu mwezi Ramadhani. Alihifadhi Qurani nzima akiwa na umri wa miaka 7 tu.
Alizaliwa mwaka 150 Hijriya (mwaka ambamo Imam Abu Hanifa aliiaga dunia), huko Asqalan au Mina au Ghizza. Aliishi Makkah na aliiaga dunia hii akiwa na umri wa miaka 53, mwaka 204 Hijriya huko Misri.
Maswali / maoni yanakaribishwa
JazakAllah.