Ads 468x60px

Jan 30, 2025

SHA'ABAAN [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo.

 

Mwezi wa nane katika Kalenda ya Kiislamu ni Sha'abaan. Utukufu wa mwezi huo juu ya miezi mingine ni kama ule wa Mtume juu ya Mitume wengine.

 

BAADHI YA TAREHE MUHIMU:

 

Qiblah ilibadilishwa kutoka Baytul Maqdis na kuwa Al Kaaba.

 

Imam Abu Hanifa, mmoja kati ya Maimamu wanne, kuiaga dunia hii tarehe 2.

 

Imam Husein RadwiyAllahu kuzaliwa tarehe 6.

 

Usiku wa kuwa huru na moto wa Jahannam (au kasimatu rizki) tarehe 15.

 

KUBADILIKA KWA QIBLAH:

 

Baytul Maqdis (Msikiti wa Aqsa) ulikuwa ndiyo Qiblah ya mwanzo ya Waislamu. Karibu Mitume wote waluielekea katika sala zao. Mtume alitamani sana kuelekea Al Kaaba tangu mwanzo tu.

 

Kila Mtume aliposali akielekea Baytul Maqdis, Mayahudi hukasirika sana na hata husema "inakuaje Mtume wenu anawaamrisheni kutenda kinyume na Mayahudi na inapokuja swala ya ibada basi anauelekea mji wetu (Jerusalem)?" Mtume hakujisikia kabisa vizuri kwa maneno hayo ya Mayahudi na alitamani sana kuelekea Al Kaabah.

Sub-Hanallah! Mara moja Allah Akatelemsha aya inayoelezea: "Tunashuhudia ukiinua uso wako mara kwa mara mbinguni. Basi tutakuelekeza upande wa Qiblah uiridhiayo wewe. Elekea Msikiti wa Haraam (Al Kaaba) sasa hivi, na enyi Waislamu! Elekeze nyuso zenu huko pia, popote mlipo .." (Quran Tukufu 2:144). Zingatieni watukufu Waislamu kuwa badiliko la Qiblah limetokea kwa sababu tu ya kumridhisha Mtume . Kuanzia hapo qiblah yetu ni Al Kaaba huko Makkah.

 

IMAM ABU HANIFA:

 

Jina lake hasa ni Nooman bin Thabit bin Zuta bin Mah. Alizaliwa katika mji wa Kufa, Iraq, mwaka wa 80 Hijria. Alikuwa katika zama tukufu wa Tabi'in (wale waliowafuata Masahaba).

 

Amepokea Abu Huraira RadwiyAllahu Anhu kuwa Mtume amesema kuwa : Katika ummah wangu atakuja mtu ataitwa Abu Hanifa. Siku ya Qiyama yeye (Abu Hanifa) ndiye atakuwa taa ya ummah wangu. Hadithi nyingine imeeleza kuwa "katika kila karne idadi Fulani ya ummah wangu utakuwa na daraja ya juu; Abu Hanifa atakuwa na daraja ya juu zaidi katika zama zake".

 

Miongoni mwa Masahaba aliokutana nao ni Sayyiduna Anas bin Maalik, Sayyiduna Sahl bin Saad na Sayyiduna Abul Tufail Amir bin Wathila RadwiyAllahu Anhum. Imam Abu Hanifa alipata elimu ya dini kupitia baadhi ya Masahaba na wanazuoni wapatao kama 4,000. Baadhi ya Masahaba ni Sayyiduna Hammad Basri, Sayyiduna Ata bin Abi Rabah, Sayyiduna Ikramah, Sayyiduna Imam Baaqir, Sayyiduna Imam Jafar Saadiq, Sayyiduna Abu Ali, Sayyiduna Abu Hurayrah, Sayyiduna Abdullah Ibn Umar, Sayyiduna Aqabah bin Umar, Sayyiduna Safwaan, Sayiduna Jabir na Sayyiduna Abu Qatadah RadwiyAllahu Anhum.

 

Imam Abu Hanifa alikuwa mfanya biashara na kila Ijumaa alikuwa akitoa sarafu 20 za dhahabu kwa wasiojiweza kama sadaka. Kwa muda wa miaka 40 Imam alisali sala ya Alfajiri kwa udhu ule ule wa sala ya Ishai (kwa maana usiku kucha alikuwa katika ibada bila ya kulala). Imam alihiji mara 55. Alihitimisha Quran Tukufu kila siku kimoja na usiku kimoja. Pia alikuwa akihitimisha Quran Tukufu katika rakaa moja ama mbili. Alikuwa mcha Mungu sana kiasi cha kufunga mwaka mzima (isipokuwa siku zile 5 zilizokatazwa) kwa muda wa miaka 30. Mahala alipofariki, alisoma Quran Tukufu 7,000.

WATUKUFU WAISLAMU TUPO JAMANI!!!

Mwezi Sha'abaan mwaka 150 Hijria, Imam aliiaga dunia hii huko Iraq akiwa katika hali ya sala, akiwa na umri wa miaka 70. Jeneza lake lilisaliwa mara 6 na kila mara waumini wapatao 50,000 walihudhuria na wengine walikuja kumuombea kwenye kaburi lake kwa siku karibu 20 hivi.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

Jan 25, 2025

Mi-iraj - PT 5 (MWISHO) [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Namalizia risala yetu kuhusu msafara wa Isra na Mi-'iraj. In sha Allah risala ya mwezi Sha-'abaan itafuata, kwani leo ni mwezi mosi Sha-'abaan. 

 

Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad , hapo juu ni aya ya 8 HADI 10 ya Sura Najmi, inayozungumzia Mtume Muhammad kuonana na Allah.

 

Mtume Muhammad alishuhudia Pepo na moto na baadae kufika Sidrah, ambapo alisikia sauti ya SUB-HANALLAH, ALHAMDULILLAH. Mtume Muhammad aliuliza ni kitu gani hiyo? Jibrail akajibu kuwa Sidrah, ambayo ni mti mkubwa, Malaika huleta dhikri. Hapo ndipo tamati ya Malaika. Mtume Muhammad alimwambia Jibrail waendelee lakini Jabirail akamjibu kuwa akisogea hatua moja kutoka hapa basi mbawa zake zitaungua kutokana na Nuru ya Allah; akamuambia Mtume Muhammad aendelee na safari.

Hapa ndipo Jibrail alimuomba idhini Mtume Muhammad ili amuonyeshe utukufu aliojaaliwa na Allah; kwani siku zote hizo Jibrail alikuwa akimjia Mtume Muhammad katika sura ya binadamu tu. Jibrail alipoondoa pazia mbawa zake 600 zikaonekana na ukubwa wa kila mbawa ulizidi hata ukubwa wa ardhi yote ya dunia. Wanazuoni wanasema lau kama Mtume Muhammad angemuonyesha utukufu wake, basi Jibrail angezimia pengine hadi kiyama.

Baada ya hapo Jibrail alimuomba Mtume Muhammad amtakie idhini kutoka kwa Allah kuwa siku ya kiyama wakati umma wake utakapopita kwenye njia nyepesi, basi yeye atande mbawa zake kuwasalimisha wapite kwa raha.

Baada ya hapo Mtume Muhammad alimpanda Rafraf na kuelekea juu zaidi. Baada ya kupita Arshi ndipo alimuona na Allah kwa macho yake, na hapo ndipo alimkaribia Allah. Kisha Allah Alimjaalia wahyi. Allah Alimuuliza je umeleta nini?

Mtume : Attahiyatu lillahi wasswalawaatu wattayyibaatu.

Allah : Assalaamu alaika ayyuhan Nabiyyu warahmatullahi wabarakaatuhu (salamu ziwe juu yako ewe Mtume pamoja na Rahma na Baraka).

Mtume : Assalaamu alaina wa-alaa ibadillahis swaalihin (salamu ziwe juu yetu na waja wako wema).

Hapo ndipo Allah Alimzawadia sala 50 za kutwa nzima. Mtume Muhammad alianza safari ya kurudi, lakini alipokutana na Mtume Musa katika mbingu ya 6, alimuambia arudi kwa Allah ili zipunguzwe kwani ummah wake walifaradhishiwa sala 2 tu kutwa nzima na walishindwa. Mtume Muhammad alirudi tena kwa Allah kutaka kupunguziwa, na Allah alimpunguzia sala 5. Alipofika tena kwa Mtume Musa, aliambiwa bado ni nyingi na kurudi tena kwa Allah. Kila nenda rudi sala 5 zinapungua hadi kusalia sala 5 na hapo ndipo Mtume Muhammad alisema sasa anaona haya kurudi tena kwa Allah. Ila Allah Alimuambia kuwa ummah wako itasali sala 5 tu lakini Sisi tutamjaalia thawabu za sala 50.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

Jan 23, 2025

Mi-iraj - PT 4 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Tunaendelea na risala yetu kuhusu msafara wa Isra na Mi-'iraj. 

 

Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad , hapo juu ni aya ya kwanza ya Sura Bani Israil, ambayo inazungumzia msafara wa miraji.

 

Tafsiri ya aya:

Utukufu ni Wake Yeye Aliyempeleka Mja Wake katika sehemu tu ya usiku kutoka Msikiti wa Haraam (Makkah) hadi Msikiti wa Aqsa (Palestina), ambao umezungukwa na Baraka Zetu, ili Tumuonyeshe baadhi ya alama zetu. Hakika Allah ndiye Mwenye Kusikia Mwenye Kuona.

 

Mtume Muhammad alipoanza safari ya Masjidul Aqsa, njiani alimuona Mtume Musa akisali ndani ya kaburi lake. Hapa tunapata kufahamu kuwa Mitume si tu wapo hai ndani ya makaburi yao, bali huwa wanasali na pia hupata rizki.

 

Mtume Muhammad alipofika Masjidul Aqsa, Jibrail alitoboa sehemu moja iitwao Sakhra na kisha kumfunga mnyama wao. Kisha Jibrail alitoa adhana juu ya Msikiti wa Sakhra na kurudi Masjidul Aqsa. Hapa Mitume wote walikuwepo na kila mmoja akawa anafikiria je ni Mtume Adam ambae ni baba wa binadamu wote, ndiye atakaesalisha leo? Au Khalili wa Allah, Mtume Ibrahim? Au ni Mtume Nuh kwani baada ya tufani ya zama zake, masuala ya uzaaji ulianza kupitia yeye. Lakini Jibrail alimshika mkono Mtume Muhammad na kumpeleka mbele na kumuambia awa imamu wa Mitume wote. Baada ya sala, kila Mtume alisoma khutba ya kumsifu Mtume Muhammad .

 

Baada ya hapo Mtume Muhammad alifuatana na Jibrail kuelekea mbinguni. Kuna riwaya 2; (1) walienda kumtumia mnyama yule yule Buraaq au (2) Miraji ni jina la ngazi mmoja na hivyo walitumia ngazi hiyo kuelekea juu. Walipofika mbingu ya 1, mlango ulikuwa umefungwa. Jibrail alipiga hodi na kuulizwa ni nani? Alijibu mimi Jibrail niko na Mtume Muhammad . Baada ya kuulizwa kama Mtume Muhammad ameitwa, Jibrail akajibu kuwa ndiyo.

 

Mtume Muhammad alimuona mzee mmoja ambae kila akiangalia vivuli upande wake wa kulia basi hutabasamu lakini anapoangalia vivuli upande wa kushoto basi hulia. Mtume Muhammad aliuliza ni nani huyo na kwa nini mara hutabasamu na mara hulia? Jibrail alijibu kuwa msalimie huyu ni mtume Adam, upande wake wa kulia ni watoto wake walioleta imani na ndyo maana hutabasamu akiwaona. Wale wa kushoto ni watoto wake waliokataa imani na ndyo maana hulia akiwaona.

 

Mtume Muhammad alianza kuchupa mbingu moja baada ya nyingine huku akikutana na Mitume kila mbingu. Mbingu wa 2 alikutana na Mtume Yahya na isa, ya 3 Mtume Yusuf, ya 4 Mtume Idris, ya 5 Mtume Harun, ya 6 Mtume Musa nay a 7 alikutana na Mtume Ibrahim aliekaa kwa kuegemea Baitul Maamur. Baitul Maamur ni kibla ya Malaika mbingu ya 7, ambamo kila asubuhi na jioni Malaika 70,000 wapya huingia hapo. Mtume Muhammad aliwasalisha Malaika.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

Jan 22, 2025

Mi-iraj - PT 3 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

Natumai hamjambo. Leo ni usiku wa Isra wal Mi-'iraj.

Picha hapo chini ni sehemu takatifu mno ndani ya Masjidul Aqsa, nchini Palistina, ambapo Mtume alianza safari yake hapo ya kwenda mbinguni. Jiwe hilo linaitwa SAKHRAA.

Jan 21, 2025

Mi-iraj - PT 2 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Tunaendelea na risala yetu kuhusu msafara wa Isra na Mi-'iraj. Ijumaa Kareem

 

 

Kwanza kabisa hebu iangalie kwa makini jiwe katika picha niliyoambatanisha. Usiku wa Mi-'iraj wakati Mtume alipoanza safari ya kupaa mbinguni pamoja na mnyama Burraq, hilo jiwe nalo likaanza kupaa. Hapo ndipo Mtume alipoiamuru kusimama, na kwa kuwa ilikuwa imeshaanza kupaa basi jiwe ikasimama hivyo hivyo hewani na hadi leo hii jiwe hilo lipo kando kidogo na Masjidul Aqsa, Palestina.

 

 

 

 

 

Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad , hapo juu ni aya ya kwanza ya Sura Bani Israil, ambayo inazungumzia msafara wa miraji.

 

Tafsiri ya aya:

Utukufu ni Wake Yeye Aliyempeleka Mja Wake katika sehemu tu ya usiku kutoka Msikiti wa Haraam (Makkah) hadi Msikiti wa Aqsa (Palestina), ambao umezungukwa na Baraka Zetu, ili Tumuonyeshe baadhi ya alama zetu. Hakika Allah ndiye Mwenye Kusikia Mwenye Kuona.

 

Imeelezwa kwenye vitabu vya Bukhari na Muslim kuhusiana na msafara huo kuwa Mtume Muhammad alikuwa nyumbani kwa Ummi Haani, kisha aliletwa sehemu inaitwa Hatim ndani ya Msikiti Mtukufu wa Makkah. Hapa alipasuliwa kifua, moyo ulitolewa na kuoshwa na maji matukufu ya zamzam na kujazwa hikma ndani yake na kisha kurudishwa na baada ya hapo kifua kikashonwa. Baada ya hapo Malaika mtukufu Jibrail Alaihissalaam alimuambia kuwa Allah Amemuita. Aliletwa mnyama mmoja aitwae Burraaq, ambae ni mkumbwa kuliko punda na mdogo kuliko farasi, aliye na kasi kiasi cha kuwa hatua yake moja umbali wake ni sawa na tamati ya sisi kuona. Mtume Muhammad alimpanda na kuanza safari ya kwenda Msikiti wa Aqsa.

 

Mtume Muhammad alionyeshwa baadhi ya alama wakati anaelekea Msikiti wa Aqsa, nazo ni kama ifuatavyo:

 

1. Mtume Muhammad aliwaona baadhi ya watu wakilima, huku wanaendelea kupanda mbegu na papo hapo mazao yalikamilika na watu hao kuvuna na kupata faida. Mtume Muhammad alifahamu kila kitu, lakini kuuliza kwake ni kwa ajili ya mafundisho kwetu.

Aliuliza: hivi ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hawa ni katika ummah wako wanaotoa katika njia ya Allah; mfano kujenga Misikiti, madrasa, nk basi hupata faida papo hapo tu.

 

2. Mtume Muhammad aliwaona watu wamelala na vichwa vyao kupondwa, kisha husima wakiwa wazima na baadae hulala na vichwa hupondwa.

Aliuliza: ni kina nani hao:

Jibrail almijibu: hao ni wale wanaopendelea kulala wakati wa sala ya Alfajiri, wanaona usingizi mtamu na pia huacha sala. Wataadhibiwa hivyo hadi siku ya Kiyama.

 

3. Mtume Muhammad aliwaona baadhi ya watu wakila mawe na miti porini lakini hawashibi.

Aliuliza: ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hao ni wale wasiotoa zaka kutokana na walichojaaliwa na Allah na pia hula haki za masikini.

Mtume Muhammad amesema kuwa toeni zaka ili mkinge mali zenu.

 

4. Mtume Muhammad aliwaona watu ambao wamewekewa vyakula mbalimbali halali na vizuri sana mbele yao, lakini wanayaacha hayo na kukimbilia kula vyakula vibaya vilivyooza na kutoa herufu mbaya.

Aliuliza: ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hao ni wale wanaowaacha wake zao halali na hukimbilia kwa wanawake wa nje na kutenda mambo ya haramu.

 

5. Mtume Muhammad alimuona mtu mmoja mwembamba sana aliyekusanya kuni nyingi. Alipotaka kuubeba akashindwa. Badala ya kupunguza kuni kidogo, akaenda porini kuongeza kuni zingine.

Aliuliza: ni nani huyo?

Jibrail alimjibu: ni yule mwenye kuleta khiyana kwenye amana za watu na pia huweka tamaa apewe amana zaidi.

 

6. Mtume Muhammad aliwaona baadhi ya watu wakikata taya zao kwa kisu kikali. Wanapomaliza za upande wa kulia na kukata za upande wa kushoto, za kulia huwa sawa.

Aliuliza: ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hao ni wale wanaoeneza fitina kwa ulimi wao.

 

Hizo ni baadhi alama alizoonyeshwa Mtume Muhammad katika msafara wake.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

 

Visitor's Traces

Total Page views