Ads 468x60px

Jan 21, 2025

Mi-iraj - PT 2 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Tunaendelea na risala yetu kuhusu msafara wa Isra na Mi-'iraj. Ijumaa Kareem

 

 

Kwanza kabisa hebu iangalie kwa makini jiwe katika picha niliyoambatanisha. Usiku wa Mi-'iraj wakati Mtume alipoanza safari ya kupaa mbinguni pamoja na mnyama Burraq, hilo jiwe nalo likaanza kupaa. Hapo ndipo Mtume alipoiamuru kusimama, na kwa kuwa ilikuwa imeshaanza kupaa basi jiwe ikasimama hivyo hivyo hewani na hadi leo hii jiwe hilo lipo kando kidogo na Masjidul Aqsa, Palestina.

 

 

 

 

 

Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad , hapo juu ni aya ya kwanza ya Sura Bani Israil, ambayo inazungumzia msafara wa miraji.

 

Tafsiri ya aya:

Utukufu ni Wake Yeye Aliyempeleka Mja Wake katika sehemu tu ya usiku kutoka Msikiti wa Haraam (Makkah) hadi Msikiti wa Aqsa (Palestina), ambao umezungukwa na Baraka Zetu, ili Tumuonyeshe baadhi ya alama zetu. Hakika Allah ndiye Mwenye Kusikia Mwenye Kuona.

 

Imeelezwa kwenye vitabu vya Bukhari na Muslim kuhusiana na msafara huo kuwa Mtume Muhammad alikuwa nyumbani kwa Ummi Haani, kisha aliletwa sehemu inaitwa Hatim ndani ya Msikiti Mtukufu wa Makkah. Hapa alipasuliwa kifua, moyo ulitolewa na kuoshwa na maji matukufu ya zamzam na kujazwa hikma ndani yake na kisha kurudishwa na baada ya hapo kifua kikashonwa. Baada ya hapo Malaika mtukufu Jibrail Alaihissalaam alimuambia kuwa Allah Amemuita. Aliletwa mnyama mmoja aitwae Burraaq, ambae ni mkumbwa kuliko punda na mdogo kuliko farasi, aliye na kasi kiasi cha kuwa hatua yake moja umbali wake ni sawa na tamati ya sisi kuona. Mtume Muhammad alimpanda na kuanza safari ya kwenda Msikiti wa Aqsa.

 

Mtume Muhammad alionyeshwa baadhi ya alama wakati anaelekea Msikiti wa Aqsa, nazo ni kama ifuatavyo:

 

1. Mtume Muhammad aliwaona baadhi ya watu wakilima, huku wanaendelea kupanda mbegu na papo hapo mazao yalikamilika na watu hao kuvuna na kupata faida. Mtume Muhammad alifahamu kila kitu, lakini kuuliza kwake ni kwa ajili ya mafundisho kwetu.

Aliuliza: hivi ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hawa ni katika ummah wako wanaotoa katika njia ya Allah; mfano kujenga Misikiti, madrasa, nk basi hupata faida papo hapo tu.

 

2. Mtume Muhammad aliwaona watu wamelala na vichwa vyao kupondwa, kisha husima wakiwa wazima na baadae hulala na vichwa hupondwa.

Aliuliza: ni kina nani hao:

Jibrail almijibu: hao ni wale wanaopendelea kulala wakati wa sala ya Alfajiri, wanaona usingizi mtamu na pia huacha sala. Wataadhibiwa hivyo hadi siku ya Kiyama.

 

3. Mtume Muhammad aliwaona baadhi ya watu wakila mawe na miti porini lakini hawashibi.

Aliuliza: ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hao ni wale wasiotoa zaka kutokana na walichojaaliwa na Allah na pia hula haki za masikini.

Mtume Muhammad amesema kuwa toeni zaka ili mkinge mali zenu.

 

4. Mtume Muhammad aliwaona watu ambao wamewekewa vyakula mbalimbali halali na vizuri sana mbele yao, lakini wanayaacha hayo na kukimbilia kula vyakula vibaya vilivyooza na kutoa herufu mbaya.

Aliuliza: ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hao ni wale wanaowaacha wake zao halali na hukimbilia kwa wanawake wa nje na kutenda mambo ya haramu.

 

5. Mtume Muhammad alimuona mtu mmoja mwembamba sana aliyekusanya kuni nyingi. Alipotaka kuubeba akashindwa. Badala ya kupunguza kuni kidogo, akaenda porini kuongeza kuni zingine.

Aliuliza: ni nani huyo?

Jibrail alimjibu: ni yule mwenye kuleta khiyana kwenye amana za watu na pia huweka tamaa apewe amana zaidi.

 

6. Mtume Muhammad aliwaona baadhi ya watu wakikata taya zao kwa kisu kikali. Wanapomaliza za upande wa kulia na kukata za upande wa kushoto, za kulia huwa sawa.

Aliuliza: ni kina nani hao?

Jibrail alimjibu: hao ni wale wanaoeneza fitina kwa ulimi wao.

 

Hizo ni baadhi alama alizoonyeshwa Mtume Muhammad katika msafara wake.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

Jan 20, 2025

Mi-iraj - PT 1

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Kama mnavyofahamu kuwa mwezi tulionao ni wa Rajab na usiku wa Jumatatu (24/4/2017) kuamkia Jumanne (25/4/2017) ni katika usiku takatifu katika historia ya Kiislam, kwani ni usiku ambamo Mtume wetu mpendwa alijaaliwa muujiza wa isra na Mi-'iraj.

Hivyo nitakuwa natuma risala fupi fupi kuhusu msafara huo in sha Allah.

 

 

 

 

Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad Swall-Allahu Alaihi Wasallam, hapo juu ni aya ya kwanza ya Sura Bani Israil, ambayo inazungumzia msafara wa miraji.

 

Ieleweke kuwa kila Mtume aliyeletwa hapa duniani alipewa muujiza au miujiza.

Lakini Mtume Muhammad Swall-Allahu Alaihi Wasallam aliletwa kama muujiza licha ya kupewa miujiza mingi, mmojawapo ukiwa huu msafara wa miraji.

 

Tafsiri ya aya:

Utukufu ni Wake Yeye Aliyempeleka Mja Wake katika sehemu tu ya usiku kutoka Msikiti wa Haraam (Makkah) hadi Msikiti wa Aqsa (Palestina), ambao umezungukwa na Baraka Zetu, ili Tumuonyeshe baadhi ya alama zetu. Hakika Allah ndiye Mwenye Kusikia Mwenye Kuona.

 

Tukiichunguza aya peke yake tu ina nukta nyingi za kuzingatia.

1. Kwanza kabisa, Allah Ametaja Utukufu Wake kwa kuanza aya. Hii ni kuukata kata kabisa utata uliotokea na utakaotokea kwani mwenye kuleta utata katika msafara huu, basi moja kwa moja analeta mashaka katika uwezo wa Sub-hana!

2. Baadhi ya watu wanadai kuwa eti Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam alioteshwa tu kwenda mbinguni na si kuwa alienda (yaani eti mwili wake haukuenda)!!! Sehemu ya pili ya aya inafafanua : "ALIYEMPELEKA MJA WAKE". Sehemu ya aya haisemi kuwa "alimuotesha"! Hivyo mwenye kupinga msafara huo wa kiwiliwili na roho basi atatoka katika Uislamu.

3. Msafara huu ulifanyika katika sehemu fupi mno ya usiku. Riwaya moja inaelezea ufupi wa msafara kuwa maji aliyotawadhia Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam yalikuwa bado yanasambaa ardhini wakati Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam aliporejea. Riwaya nyingine inasema kuwa Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam alipofungua mlango kutoka chumbani mwake, ile komeo (cheni) bado ilikuwa ikicheza aliporejea! Kwa ufupi hatuwezi kupata picha ya ufupi wa msafara huo na ndiyo maana ikatajwa kuwa ni muujiza.

4. Vile vile ni sababu ya msafara kuwa usiku tu? Sababu kuwa iliyotajwa kuwa ili watu wasipate kuona. Imani ni kuamini kisichoonekana, hivyo lau kama msafara ungetokea mchana basi wengi wangemuona Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam akienda na hivyo kupima imani ingekuwa ngumu.

5. Kwa nini sehemu ya kwanza ya msafara ulikuwa kutoka Makkah hadi Palestina? Hii ni kwa sababu Waarabu walikuwa na misafara ya mara kwa mara baina ya sehemu hizo. Hivyo kuwafahamisha kuwa msafara huu wa Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam baina ya sehemu hizo katika muda mfupi ili wawe na picha ya sehemu wanazoambiwa.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

Jan 5, 2025

RAJAB-UL-MURAJJAB - PT 4 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Mwezi 6 Rajab mmoja katika kiongozi wa masharifu kwa tarika ya Chishti aliiaga dunia na ifuatayo ni risala fupi.

 

 

SULTAN MUINUDDIN CHISHTI RAHIMAHULLAH.

 

Sultan Muinuddin Chishti Rahimahullah alizaliwa Khorasan, Afghanistan. Alikuwa mwaka sambamba na Sayyid AbdulQadir Jilani Qaddasallahu Sirrah. Kwa kuwa Sayyid AbdulQadir Jilani Qaddasallahu Sirrah alishachaguliwa kuiongoza bara la Uarabuni kuhuisha dini, Mtume alimchagua Sultan Muinuddin Chishti Rahimahullah kuiongoza bara Hindi katika kuinusuru dini. Hakuwahi kupita maeneo ya bara Hindi wala hakufahamu kabisa lugha ya kihindi. Mtume alimjia kwenye ndoto na kumuonyesha njia ya kwenda bara Hindi na kisha alimtemea mate matukufu na hivyo akafahamu lugha ya kihindi kwa fasaha.

 

Kutokana na karama zake, wachawi wa kibaniani wakajua huo ni uchawi, hivyo mfalme wa huko aliwakusanya wachawi wakubwa kukabiliana nae lakini wote walishindwa na hatimaye kusilimu. Zaidi ya mabaniani milioni 9 walisilimu kutokana na karama zake tofauti. Hatimaye aliiaga dunia mwezi 6 Rajab.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa

 

JazakAllah.

Jan 3, 2025

RAJAB-UL-MURAJJAB - PT 3 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Mwezi 4 Rajab ambamo mmoja katika maimamu wetu wane, Imam Shafi-'I aliiaga dunia.

 

 

Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad , aya hapo juu ya 36 ya Sura Tawbah, inazungumzia utukufu wa miezi minne. Mwezi Rajab, ambao ni mmojawapo kati ya miezi hiyo minne, mwezi ambao una fadhila tele. Ni mwezi ambamo dua hukubalika.

TAFSIRI: Bila shaka idadi ya miezi kwa Allah ni miezi kumi na mbili katika kitabu cha Allah tangu Alipoumba mbingu na ardhi, miongoni mwao minne ni yenye huruma (tukufu). Hii ni dini iliyonyooka na hivyo msidhulumu nafsi zenu katika miezi hizo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wanavyopigana nanyi nyote, na jueni kuwa Allah yu pamoja na wachamungu.

 

IMAM SHAFI-'I RAHIMAHULLAH.

Jina la Imam Shafi-'I ni Muhammad bin Idris bin Abbas bin Uthman bin Shafi-'I bin Saib bin Ubeid bin Abdi Yazid bin Hashim bin Abdul Muttalib bin Abdi Manaf.

 

Abdi Manaf ni katika ukoo wa nne wa Mababu zake Mtume . Ukoo wa Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam uko hivi: (Sayyidina) Muhammad bin Abdullah bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdi Manaf. Hivyo Mtume amezaliwa kupitia mwanae Abdi Manaf (Hashim) wakati Imam Shafi-'I amezaliwa kupitia Abdul Muttalib.

Imam Shafi-'I amekuwa maarufu kwa jina hilo (Shafi-'i)  kupitia kwa babu yake katika ukoo wa tatu (Shafi-'i).

 

Wazazi wake wanatokana na kabila maarufu la kiarabu la Bani Hashim. Baadhi ya sababu ya yeye kuwa na kipaji hicho ni kuwa alikuwa : Imam (kiongozi – wa Dini), Mwanasheria (wa masuala ya sharia za Dini), Mcha Mungu na mtu mwenye hekima na busara. Alikuwa mwandishi wa vitabu vikubwa 14 vya kanuni na falsafa vya sharia ya Kiislam na pia vitabu vingine vidogo zaidi ya 100.

 

Kila alipopatwa na tatizo, Imam Shaifi-'I alielekea Baghdad kudhuru kaburi la Imam Abu Hanifa, kisha husali rakaa 2 na kumuomba Allah kupitia (wasila) kwa Imam Abu Hanifa. Imam Shafi-'I mwenyewe amesema kuwa hakika maombi yanakubalika katika kaburi la Imam Abu Hanifa.

 

Imam Shafi-'I alikuwa mwanafunzi wa Imam Malik Radwiy-Allahu Anhu. Alikuwa akihitimisha Quran (Msahafu) nzima katika usiki moja tu mwezi Ramadhani. Alihifadhi Qurani nzima akiwa na umri wa miaka 7 tu.

 

Alizaliwa mwaka 150 Hijriya (mwaka ambamo Imam Abu Hanifa aliiaga dunia), huko Asqalan au Mina au Ghizza. Aliishi Makkah na aliiaga dunia hii akiwa na umri wa miaka 53, mwaka 204 Hijriya huko Misri.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa

 

JazakAllah.

Jan 1, 2025

RAJAB-UL-MURAJJAB - PT 2 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo. Mwezi wa Rajab tumeshauanza na ifuatayo ni sehemu ya kwanza ya risala …

 

 

Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad , aya hapo juu ya 36 ya Sura Tawbah, inazungumzia utukufu wa miezi minne. Mwezi Rajab, ambao ni mmojawapo kati ya miezi hiyo minne, mwezi ambao una fadhila tele. Ni mwezi ambamo dua hukubalika.

TAFSIRI: Bila shaka idadi ya miezi kwa Allah ni miezi kumi na mbili katika kitabu cha Allah tangu Alipoumba mbingu na ardhi, miongoni mwao minne ni yenye huruma (tukufu). Hii ni dini iliyonyooka na hivyo msidhulumu nafsi zenu katika miezi hizo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wanavyopigana nanyi nyote, na jueni kuwa Allah yu pamoja na wachamungu.

                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                   

Mwezi wa saba katika kalenda ya Kiislam inaitwa RAJAB, ambayo inatokana na neno "TARJIB", yenye maana ya heshima na hata zama za ujahili Waarabu waliuheshimu sana mwezi huu kwa kuacha mapigano na mauaji, wakisema ni mwezi wa Mwenyezi Mungu.

Mtume amesema kuwa Rajab ni mwezi wa Allah, Shaaban ni wa kwangu na Ramadhani ni ya ummah wangu.

 

Mtume amesema kuwa Rajab ni mwezi wenye fadhila nyingi, thawabu ya amali njema huwa maradufu ya thawabu ya kawaida. Mwenye kufunga swaum 1 ndani ya Rajab, basi ni sawa na kufunga mwaka mzima.

Siku 1 Mtume Isa Alaihissalaam alipokuwa akipita karibu na mlima mmoja, aliona nuru sehemu Fulani ya mlima. Alimuomba idhini Allah ili aweze kuzungumza na mlima. Mlima ilimuuliza nini atakacho?  Mlima ikasema kuwa ndani yake kuna Mcha Mungu mmoja nan i kwa sababu ya huyo mlima una nuru. Mtume Isa Alaihissalaam alimuomba Allah aonyeshwe huyo mtu na mara mlima ikapasuka na akaonekana Mcha Mungu aliye mzuri sana. Alisema kuwa yeye ni katika watu wa Mtume Musa Alaihissalaam na alimuomba Allah Amjaalie maisha marefu ili aweze kushuhudia zama za Mtume wa mwisho Muhammad na hivyo ahesabiwe miongoni mwa ummah wa Mtume wa mwisho. Mcha Mungu huyo alikuwa mlamani humo kwa miaka 600. Kisha Mtume Isa alimuuliza Allah kama kuna Mcha Mungu ardhini zaidi ya huyo bwana? Allah alimjibu: "Ewe Isa, lau kama mja wangu katika ummah wa Mtume wa mwisho akifunga siku moja tu ya mwezi Rajab, basi huyo mja kwangu atakuwa Mcha Mungu zaidi kuliko huyo bwana!! (SUB-HANALLAH).

 

Baadhi ya tarehe muhimu:

Tarehe 1 – Mtume Nuh Alaihissalaam alianza safari na wafuasi wake katika mashua (meli) waliyoitengeneza.

Tarehe 4 – Vita vya Safin

Tarehe 4 – Imam Shafi-I Rahmatullahi Alaihi kuiaga dunia

Tarehe 6 – Sayyidina Moinuddin Chishti (kiongozi wa Walii kwa twariqa ya Chishtiya) kuiaga dunia

Tarehe 27 – Msafara wa isra na Mi-iraj ya Mtume .

 

 

 

Tarehe 1 Mtume Nuh na wafuasi wake walianza safari katika meli kabla ya tufani kali iliyowaangamiza waliompinga.

 

 

Tarehe 4: Imam Shafi aliaga dunia. Jina lake ni Muhammad bin Idris na kizazi chake cha 4 kinakutana na kile cha Mtume Muhammad kwa Abdi Manaf. Amezaliwa mwaka 150 hijria na kufariki mwaka 204h mjini Cairo, Misri. Alikuwa akikhitimisha msahafu mmoja kila siku katika mwezi Ramadhani. Kila alipopatwa tatizo, basi huenda kuizuru kaburi la Imam Abu Hanifa na kisha huomba dua akimtawassul.

 

 

 

Tarehe 6: Walii mkubwa wa Allah Moinuddin Chishti aliaga dunia nchini India. Walii huyo alikuwa mwaka sambamba na Sheikh Abdul Qadir Jilani Qaddasallahu Sirrah. Mtume Muhammad alimjaalia uwalii wa bara hindi. Mabaniani milioni 9 walisilimu kwa jitihada zake.

 

 

Tarehe 27: Msafara wa Isra na miraj ya Mtume Muhammad ambayo insha Allah tutaanza kuizungumzia hapo baadae.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa

 

JazakAllah.

 

Visitor's Traces

Total Page views