Ads 468x60px

Nov 11, 2014

Imam Hussain Radi Allahu Anhu - PT 2 (Kiswahili)


Natumai hamjambo. Namalizia risala fupi kuhusu kuuawa shahidi kwa mjukuu wa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, Imam Hussein RadwiyAllahu Anhu.



Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi wasallam, aya hapo juu ya 169 kutoka Sura Aali Imran (3), inazungumzia wanaouawa katika njia ya Allah.

TAFISIRI: Wala usiwadhanie waliouawa katika njia ya Allah kuwa wafu, bali wako hai na wanaruzukiwa kutoka kwa Mola wao Mlezi.

Imam Husein alimtuma binamu yake, Muslim bin Aqeel, pamoja na wanae wawili. Kufika huko alipokelewa kwa shangwe sana na Waislam wapatao 40,000 walimuunga mkono na kumtaka Imam Husein aje haraka sana.  Muslim bin Aqeel alimwandikia barua Imam Husein na kumtaka aanze safari mara tu apatapo burua hiyo. Hata hivyo, siku mjumbe anapotoka Kufa na barua kuelekea Makkah, huku nyuma Waislam wote 40,000 waliomuunga mkono Muslim bin Aqeel, walimtenga. Kitendo chao hicho kilimsikitisha mno Muslim na hasa ni kwa sababu alishatuma barua ya kumtaka Imam Husein aje haraka sana.

Hali hii ya Waislam hao ilitokana na taarifa kumfikia Yazid kuwa Imam Husein amemtuma mjumbe wake kupata kura ya utii, na hivyo aliwaamuru watu wake kuwatishia amani kila atakaemuunga mkono Imam Husein. Muslim akabaki peke yake na wanae wawili na kila alipoenda, Waislam walimtenga kwa hofu ya kuuliwa na watu wa Yazid. Hatimaye wanae walikamatwa na kuuliwa na hata Muslim mwenyewe aliuliwa na watu wa Yazid.

Imam Husein alipopokea barua, alinza kufunga safari ya kwenda Kufa na licha ya kushauriwa na masahaba kuwa wao walikosa imani juu ya Waislam hao wa Kufa, lakini Imam aliwakumbusha hukumu ya sheria pindi unapoitwa na Waislam. Msafara wake ulikuwa na watu 72, wakiwemo kina mama na watoto pia. Walipokuwa njiani waliletewa taarifa kuwa Waislam wa Kufa hawako pamoja nae kwani wameshamuua Muslim pamoja na wanae wawili na kumtaka arudi tena. Imam hata hivyo aliendelea na safari hadi alipofika katika kitongoji kiitwacho KARBALA, ambapo alizuiliwa na baada ya kuambiwa jina la kitongoji hicho tu alijua kuwa kauli ya Babu yake (Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam) itasadikika. Imam Husein alipokuwa mtoto, aliambiwa na Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam kuwa atauawa shahidi na Waislam katika kitongoji cha Karbala.

Hapo ndipo watu wa Yazid walimuambia kuwa aidha ampe kura ya utii yazid au ajiandae kwa vita. Imam aliwaambia kuwa yeye hakujipendekeza kuja mwenyewe bali amealikwa na miongoni mwao na kama hawataki kumuunga mkono, basi aruhusiwe kurudi tena Makkah. Lakini watu wa Yazid wakashikilia moja tu – aidha ampe kura Yazid au ajiandae kwa vita. Walipoona Imam hayupo tayari kwa kura, basi walianza vita wenyewe na kuanza kuwaua watu waliofuatana na Imam Husein. Hawakuangalia kama kuna mtoto wa miezi 6 au vijana wadogo au nani na hatimaye walimuua hata na Imam Husein kwa kumkata shingo na kisha kupitisha farasi juu ya mwili wa Imam. Walichukua kichwa cha Imam Husein na panga lao na kuanza kuzunguka mitaa ya Karbala. Dada yake na Imam Husein, Zainab, aliwaona baadhi yao wakijipiga kifua kusikitika lakini aliwaambia kuwa wanachosikitika kwa sasa ni bure tu na Allah atawafanya wakijipiga kifua hivyo hivyo tu hadi siku ya Qiyama.

Maswali / maoni yanakaribishwa.

JazakAllah,
Kind Regards,
Muhammad Khatri

0 comments:

Post a Comment

Enter your Comment here...

 

Visitor's Traces

Total Page views