Tunaendelea na risala yetu, na labda tu niwakumbushe kuwa tuliishia pale Sheikh alipoletwa mbele ya jambazi kuu kutaka kufahamu kama kweli ana pesa (dinari 40).
Jambazi kuu akamuuliza Sheikh kuwa licha ya kufahamu hao ni wanyan’ganyi, hivyo kwa nini aliwaonyesha pesa zote hizo? Sheikh aliwajibu kuwa alimuahidi mama yake kabla ya kuanza safari kuwa daima atasema ukweli tu. Jambazi kuu alianza kulia na kusema kuwa wewe kijana umemuahidi mama yako mara moja tu na unatekeleza ahadi yako, sisi kila siku tunatoa ahadi ya uongo kwa Mola wetu na hatuzitekelezi. Hapo ndipo jambazi kuu alitubu kwa makosa yake na wenzake pia walimfuatiliza na wote wakaacha ujambazi. Historia inasema kuwa wote hao wakawa Walii wa Allah siku za mbele.
Sheikh alikuwa mkarimu sana na hivyo aliwasaidia sana wanafunzi wenzake wenye hali duni. Kwa kuwa umasikini ulienea zama hizo, na baada ya Sheikh kumaliza pesa zake, alikuwa akienda porini kula aidha majani au mizizi ya baadhi ya mimea yenye kutoa maji. Sheikh alikaa siku kadhaa katika ibada ya Allah bila ya kula wala kunywa, kisha husikia sauti (ya Allah) ikimwambia “ewe AbdulQadir kunywa” na “ewe AbdulQadir kula”, ndipo hula na kunywa.
Kuna karama nyingi zilizodhihirika kupitia kwa Sheikh, mmojawapo ikiwa kuhudhuria sehemu 70 za mwaliko kwa wakati mmoja tu!! Vile vile mawaidha yake yalihudhuriwa na watu wapatao 70,000 kwa wakati mmoja. Enzi hizo hapakuwepo na vipaza sauti na hivyo desturi ilikuwa hivi; mmojawapo katika waliohudhuria husimama pale ambapo sauti humfikia na kisha huwasimulia wenzake walio nyuma. Lakini karama nyingine ya Sheikh ni kuwa Yule aliyekaa mwisho husikia kama anavyosikia aliyekaa mbele ya Sheikh! Allah amemuahidi Sheikh kuwa mfuasi wake hatakufa hadi ajaaliwe toba.
Habari za Sheikh ni nyingi mno na kwa nini isiwe hivyo kwani yeye ndiye kiongozi wa Mawalii wote wa Allah. Pia ikumbukwe kuwa karama za Mawalii (hata za umma zilizopita) zimo ndani ya Quran Tukufu. Pia ieleweke kuwa jambo lolote ambalo akili haikubaliani nalo, linapotendwa na Mitume basi huitwa MUUJIZA, na jambo la namna hiyo inapotendwa na Masahaba au Mawalii basi huitwa KARAMA.
Maswali/ maoni yanakaribishwa
JazakAllah,
Mar 13, 2013
Sheikh Sayyid AbdulQadir Jilani - PT3 (Kiswahili)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Abdul qadir na shekhe idrisa bin saadi Nani yuko juu zaidi kwa karama
ReplyDelete