Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo.
Mfungo tuliyonao ni wa Saba (Rabi-ul-Akhar), ambamo kiongozi wa Mawalii (Masharifu) – Shaikh Sayyid AbdulQadir Jilani RadwiyAllahu Anhu – aliiaga dunia. Ifuatayo ni sehemu ya kwanza ya risala fupi.
Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi wasallam, imesomwa aya ya Sura Yunus, inayozungumzia mawalii wa Allah na ndiyo itakuwa mada yetu leo kwani huu ni Mfungo 7 au Rabi ul Akhar, ambamo kiongozi wa Mawalii, Sheikh AbdulQadir Jilani aliiaga dunia.
AYA: Jihadharini, marafiki wa Allah hawana hofu wala huzuni.
Sh AbdulQadir alizaliwa Ramadhani mosi na siku hiyo walizaliwa watoto wa kiume 1,100 na wote wakawa Mawalii wa Allah. Karama yake ilidhihirika papo hapo kwani yeye hakunyonya muda wa kufunga saumu hadi muda wa futari. Habari hizi zikawa maarufu kiasi cha kwamba mwaka uliofuata kulitokea hitilafu katika mwezi. Hivyo ilishauriwa kwenda nyumbani kwa Sh AbdulQadir ili wamuulize mama yake kama mwanae amenyonya leo au la? Jibu ilikuwa hapana na hivyo ikaamuliwa kuwa mwezi uliandama.
Akiwa mtoto mdogo, Sh AbdulQadir alijitenga na mambo ya kucheza ambayo watoto wengine huwa ni kawaida kucheza. Sh AbdulQadir alikuwa akifanya ibada ya Allah na alipowaona watoto wakicheza na hujisikia kuungana nao, basi husikia sauti ikisema : “njoo kwangu ewe uliyetukuka”. Siku za mwanzo baada ya kusikia sauti hukimbia kwa mama lakini kadri siku zilipoenda alizoea na hujishughulisha katika ibada. Alipofika umri wa miaka 5, mama yake alimuandikisha katika Madrassa moja ya Jilan. Pindi Sheikh alipofika Madrassa, basi Malaika husema “mpisheni Walii wa Allah”. Alipofika umri wa miaka 18, alimuomba idhini mama yake kwenda kusoma mjini Baghdad. Zama hizo watu walikuwa wakisafiri kwa miguu ama ngamia na njia nyingi hukatiza porini ambapo wanyang’anyi hujificha. Mama alimuombea na kumpatia dinari 40 (thamani ya pesa nyingi mno zama hizo), alizomshonea kwenye koti lake, kisha akamuusia daima aseme ukweli tu. Sheikh akamuahidi mama daima atasema kweli na baada ya kuombewa akaanza safari pamoja na msafara (kama ilivyo kawaida ya zama hizo).
Baada ya kupita vijiji kama viwili, msafara ulivamiwa na majambazi. Kila alichonacho (chenye thamani) walinyan’ganywa. Majambazi walipomfikia Sheikh, wakamuuliza alichonacho, alijibu ana dinari 40. Majambazi wakampuuza kwa kufikiria kuwa kijana anawatania tu. Majambazi walipokutana kwa kiongozi wao wakiwasilisha walichonyan’ganya, wakasema kuna kijana anadai eti ana dinari 40. Kiongozi akaamuru aletwe huyo kijana na kuanza kumhoji kuhusu hizo pesa. Sheikh akawaambia alikoficha.
Jambazi kuu akamuuliza Sheikh kuwa licha ya kufahamu hao ni wanyan’ganyi, hivyo kwa nini aliwaonyesha pesa zote hizo? Sheikh aliwajibu kuwa alimuahidi mama yake kabla ya kuanza safari kuwa daima atasema ukweli tu. Jambazi kuu alianza kulia na kusema kuwa wewe kijana umemuahidi mama yako mara moja tu na unatekeleza ahadi yako, sisi kila siku tunatoa ahadi ya uongo kwa Mola wetu na hatuzitekelezi. Hapo ndipo jambazi kuu alitubu kwa makosa yake na wenzake pia walimfuatiliza na wote wakaacha ujambazi. Historia inasema kuwa wote hao wakawa Walii wa Allah siku za mbele.
Maswali / maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...