Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo. Kabla ya kuendelea na risala yetu ya Mi-‘iraj, ndugu yetu mmoja ameuliza swali na jibu lake ni hili:-
SWALI: Imamu wa Msikiti alipitisha mchango wa kuchangia ujenzi wa msikiti, waumini walichanga 35,000/- tu. Ghafla majambazi wakaingia na kuuteka Msikiti na kuamrisha kila mtu atoe alichonacho mfukoni. Wakakusanya mil 8.2, baadae wakamkabidhi imamu ili aendeleze ujenzi wa Msikiti. Je nani ana dhambi majambazi au waumini?
JIBU: Majambazi wana dhambi na pia imamu hapaswi kutumia pesa hizo kwani zimekusanywa pasipo na radhi ya waumini.
Tunaendelea na kisa cha Mi-‘iraj
SUB-HANALLADHI ASRA BI-ABDIHI LAYLAN MINAL MASJIDIL HARAAMI ILAL MASJIDIL AQSA, ALLADHI BAARAKNA HAWLAHU LINURIYAHU MIN AYATINA, INNAHU HUWAS SAMIUL BASIR. (SURA BANI ISRAIL, AYA 1)
Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam, aya hapo juu ni ya kwanza ya Sura Bani Israil, ambayo inazungumzia msafara wa miraji.
Tafsiri ya aya:
Utukufu ni Wake Yeye Aliyempeleka Mja Wake katika sehemu tu ya usiku kutoka Msikiti wa Haraam (Makkah) hadi Msikiti wa Aqsa (Palestina), ambao umezungukwa na Baraka Zetu, ili Tumuonyeshe baadhi ya alama zetu. Hakika Allah ndiye Mwenye Kusikia Mwenye Kuona.
Imeelezwa kwenye vitabu vya Bukhari na Muslim kuhusiana na msafara huo kuwa Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam alikuwa nyumbani kwa Ummi Haani, kisha aliletwa sehemu inaitwa Hatim ndani ya Msikiti Mtukufu wa Makkah. Hapa alipasuliwa kifua, moyo ulitolewa na kuoshwa na maji matukufu ya zamzam na kujazwa hikma ndani yake na kisha kurudishwa na baada ya hapo kifua kikashonwa. Baada ya hapo Malaika mtukufu Jibrail Alaihissalaam alimuambia kuwa Allah Amemuita. Aliletwa mnyama mmoja aitwae Burraaq, ambae ni mkumbwa kuliko punda na mdogo kuliko farasi, aliye na kasi kiasi cha kuwa hatua yake moja umbali wake ni sawa na tamati ya sisi kuona. Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam alimpanda na kuanza safari ya kwenda Msikiti wa Aqsa.
Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam alionyeshwa baadhi ya alama wakati anaelekea Msikiti wa Aqsa, nazo ni kama ifuatavyo:
- Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam aliwaona baadhi ya watu wakilima, huku wanaendelea kupanda mbegu na papo hapo mazao yalikamilika na watu hao kuvuna na kupata faida. Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam alifahamu kila kitu, lakini kuuliza kwake ni kwa ajili ya mafundisho kwetu.
Aliuliza: hivi ni kina nani hao?
Jibrail alimjibu: hawa ni katika ummah wako wanaotoa katika njia ya Allah; mfano kujenga Misikiti, madrasa, nk basi hupata faida papo hapo tu. Labda niongeze tu kuwa michango ya umoja wetu hapa Bollore ni mfano mzuri kwa hili. - Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam aliwaona watu wamelala na vichwa vyao kupondwa, kisha husima wakiwa wazima na baadae hulala na vichwa hupondwa.
Aliuliza: ni kina nani hao:
Jibrail almijibu: hao ni wale wanaopendelea kulala wakati wa sala ya Alfajiri, wanaona usingizi mtamu na pia huacha sala. Wataadhibiwa hivyo hadi siku ya Kiyama. - Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam aliwaona baadhi ya watu wakila mawe na miti porini lakini hawashibi.
Aliuliza: ni kina nani hao?
Jibrail alimjibu: hao ni wale wasiotoa zaka kutokana na walichojaaliwa na Allah na pia hula haki za masikini.
Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam amesema kuwa toeni zaka ili mkinge mali zenu. - Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam aliwaona watu ambao wamewekewa vyakula mbalimbali halali na vizuri sana mbele yao, lakini wanayaacha hayo na kukimbilia kula vyakula vibaya vilivyooza na kutoa herufu mbaya.
Aliuliza: ni kina nani hao?
Jibrail alimjibu: hao ni wale wanaowaacha wake zao halali na hukimbilia kwa wanawake wa nje na kutenda mambo ya haramu. - Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam alimuona mtu mmoja mwembamba sana aliyekusanya kuni nyingi. Alipotaka kuubeba akashindwa. Badala ya kupunguza kuni kidogo, akaenda porini kuongeza kuni zingine.
Aliuliza: ni nani huyo?
Jibrail alimjibu: ni yule mwenye kuleta khiyana kwenye amana za watu na pia huweka tamaa apewe amana zaidi. - Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam aliwaona baadhi ya watu wakikata taya (jaws) zao kwa kisu kikali. Wanapomaliza za upande wa kulia na kukata za upande wa kushoto, za kulia huwa sawa.
Aliuliza: ni kina nani hao?
Jibrail alimjibu: hao ni wale wanaoeneza fitina kwa ulimi wao.!
Hizo ni baadhi alama alizoonyeshwa Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam katika msafara wake, ambazo zinahusiana na maisha yetu ya kila siku.
Maoni / maswali yanakaribishwa.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...