Natumai hamjambo na mmepata bahati ya kujumuika katika shamra shamra za Maulidi (mazazi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam.
Tunaendelea na risala kuhusiana na sifa za Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam kama ilivyo ndani ya Quran na Hadithi na pia masuala ya wapingao Maulidi.
Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi wasallam, aya hapo juu ya 128 kutoka Sura At Tawbah (9), inayozungumzia kuletwa kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam.
TAFISIRI: Hakika amekujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe, yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni, anakuhangaikieni sana; kwa waumini ni Mpole nan a mwenye huruma.
HISTORIA YA KUSHEREHEKEA NA KUADHIMISHA MAULIDI YA MTUME SWALLALLAHU ALAIHI WASALLAM.
Wanaopinga Maulidi daima huwadanganya Waislamu kwa kusema kuwa eti hakuna dalili yoyote ya kusherehekea Maulidi bali hiyo imebuniwa hivi karibuni tu. Siyo hivyo tu bali husema pia kuwa eti kushurehekea Maulidi ni kama kuwaiga wakristo katika kusherehekea krismasi!! Watu hao wanatakiwa wachunguze historia sahihi na kurejea kwa Allah mara moja. Zifuatazo ni baadhi tu ya matukio yaliyonukuliwa:-
1) Mwanachuoni maarufu Mulla Ali Qari ameandika tabia ya watu wa Madina na kuandika: Watu wa Madina walikuwa wakiandaa na kuhudhuria mikusanyiko ya Maulidi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam kwa furaha na mapenzi makubwa.
2) Mwanachuoni mwingine Ibn Jauzi anasema: Watu wa Makkah na Madina, Misri, Yemen, Syria na wa Miji ya Mashariki na Magharibi ya Uarabuni walikuwa wakiandaa hafla ya kusherehekea mazazi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam. Walianza kusherehekea pindi tu mwezi ya Mfungo Sita (Rabi ul Awwal) huandama, basi huoga na kisha huvaa vazi waliopenda mno, hupaka manukato, hutoa sadaka kwa furaha na hujitahidi kusikiliza Maulidi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam. Kwa kufanya hivyo, waliambulia mafanikio makubwa, kama ilivyothibitishwa kuwa faida kubwa hupatikana mwaka mzima katika kusherehekea Maulidi, faraja na amani, njia mbalimbali za uchumi, ongezeko la watoto na mali, amani katika miji na ridhaa na amani majumbani.
3) Mwanachuoni mwingine Sheikh Yusuf bin Ismail An Nabahani amesema: Kila mwaka, wakazi wa Makkah walikusanyika mahali alipozaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam usiku wa kuamkia mazazi yake.
4) Katika kitabu cha “Fuyudh al Haramain” imeelezwa: Maulidi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam yalisherehekewa na watu wa Makkah ambao walipata Baraka nyingi kwa hilo.
5) Katika gazeti la Al Qibla ya Makkah imeelezwa: Usiku wa kuamkia Maulidi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam sherehe hufanyika Makkah na wakazi wa Makkah huita siku hiyo kuwa YAUM AL EID MAULUD UR RASULULLAH SWALLALLAHU ALAIHI WASALLAM (siku ya Idi ya Maulidi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam). Watu hupika chakula. Mkuu wa Mji wa Makkah na Kamanda wa jeshi pamoja na jeshi lao hukusanyika mahala pa kuzaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam na husoma Qasida. Mishumaa huwashwa katika mstari mmoja kutoka Msikiti Mtukufu wa Makkah hadi mahala pa kuzaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, maduka na nyumba njiani hapo pia hupambwa. Watu husoma Qasida kutwa nzima. Mwezi 11 Rabi ul Awwal usiku baada ya Sala ya Isha-I mkusanyiko wa Maulidi hufanyika. Kuanzia Sala ya Maghrib ya mwezi 11 Rabi ul Awwal hadi Sala ya Al-Asri ya mwezi 12 Rabi ul Awwal, baada ya kila sala, salamu na mizinga 21 huwasilishwa (hufyatuliwa).
6) Mwanahistoria wa karne ya 7, Sheikh Abu Al Abbas Al Azafi, na mwanae, Abu Al Qasim Al Azafi, wameandika kwenye kitabu chao Al Durr Al Munazzam : Mahujaji wachamungu na wasafiri wamethibitisha kuwa siku ya Maulidi, hakuna shughuli inayofanyika mjini Makkah – si kununua wa kuuza – isipokuwa watu wanajishughulisha kuhudhuria sehemu takatifu alimozaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam. Siku hiyo Al Kaaba hufunguliwa na watu huizuru.
Ibm Batuta nae, mwanahistoria wa karne ya 8, anaandika katika kitabu chake “Rihla” kuwa: Baada ya kila sala ya Ijumaa na siku ya Maulidi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, Mlango wa Al Kaaba hufunguliwa na kiongozi wa Banu Shayba – kabila iliyohifadhi funguo wa Mlango wa Al Kaaba – na siku ya Maulidi, Jaji Mkuu wa Makkah wa Shafi-I, Najm-al-Din Muhammad ibn Al-Imam Muhyi Al-Din Al-Tabari, hugawa chakula kwa ukoo wa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam na kwa watu wa Makkah.
Maswali / maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...