Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo. Kwanza kabisa mtaniwia radhi kwa kukaa kimya kwa zaidi ya miezi miwili na tumekosa sana darsa muhimu za miezi hizo. Insha Allah, nitajitahidi kuzingatia muda.
Pili huu ni Mfungo 6 au mwezi wa Rabi-ul-Awwal au mwezi wa Maulidi au pia mwezi wa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, hivyo kuna mada nzito na nyeti za kusimulia na insha Allah nitajitahidi kufanya hivyo ili sote tufaidike.
Kwa kuanza tu, ifuatayo ni risala fupi tu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam.
Mtume wetu mpendwa Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam alizaliwa alfajiri ya Jumatatu ya mwezi 12 Mfungo 6 (Rabi ul Awwal), mwaka wa tembo (Aprili 20, 571). Unaitwa mwaka wa tembo kwa sababu mfalme wa Yemen, Abraha (mkristo), alituma jeshi la tembo kuvunja Al-Kaaba – Nyumba Tukufu ya Allah. Abraha alijenga nyumba nzuri ya ibada ya masanamu huko Sana’a, Yemen yenye dhamira ya watu kuacha kwenda kuabudu sanamu kwenye Al-Kaaba. Hakufaulu na dhamira yake kwani watu wake wenyewe walipendelea kwenda Al-Kaaba kuabudu sanamu. Jambo hili ilimchukiza sana na hivyo akawaandaa wanajeshi na tembo kwenda kuvunja Al-Kaaba. Walipokaribia tu Al-Kaaba, msaada wa Allah ulidhihirika: ghafla tu tembo walikaa chini na kukataa ketembea, mbinguni kukawa kweusi, halaiki ya ndege wachanga waliobeba mawe mdomoni na miguuni waliporomosha mawe hayo juu ya wanajeshi na tembo ambayo iliwasaga na karibu wote, akiwemo Abraha mwenyewe, walikufa papo kwa hapo. SUB-HANALLAH, hivi ndivyo Allah Alivyohifadhi Nyumba Yake Tukufu dhidi ya maadui zake.
Baba wa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, aliyefariki kabla ya Mtume kuzaliwa, anaitwa Abdullah RadwiyAllahu Anhu na mama ni Amina RadwiyAllahu Anha. Ukoo wake ni Bani Hashim na kabila ni Quraish. Alipozaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam mjini Makkah, miujiza mingi ilidhihirika maeneo yake na ulimwenguni kwa ujumla; mfano: masanamu yaliyowekwa ndani ya Al-Kaaba kuanguka, moto wa uajemi kuzimika ghafla, mama Amina RadwiyAllahu Anha kuona yoliyotokea duniani upande wa mashariki hadi mwisho na magharibi hadi mwisho, n.k. Ilikuwa desturi ya kinamama wa kabila kubwa kama Quraish kuwapeleka watoto wao wachanga kulelewa vijijini kwenye jangwa kwa malazi bora kiafya na kimwili. Hali ya mama Amina RadwiyAllahu Anha kifedha ilikuwa duni mno na hivyo kuwashuhudia walei wazuri wa kabila ya Banu Saad wakiwachukua watoto wa matajiri na hakuna aliyemuulizia Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam. Mama Halima RadwiyAllahu Anha alikuwa miongoni mwa walei hao. Hata hivyo, alikuwa masikini, mwenye afya duni na hakuwa hata na maziwa ya kutosha kwa ajili ya mwanae; hata ngamia na punda wao walikuwa na afya duni. Katika hali hiyo hakuna mama aliyekubali mwanae kulelewa na mama Halima RadwiyAllahu Anha. Mama Halima RadwiyAllahu Anha hakutaka kurudi mikono mitupu. Alisikia kuhusu mtoto wa Quraish (Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam) na alimwendea mama Amina RadwiyAllahu Anha kumuomba apewe mtoto wake kumlea na kisha wakakubaliana.
Maswali/ maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Kind Regards,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...