Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo na mnaendelea na matayarisho ya kusherehekea na kuadhimisha siku Tukufu ya kuzaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, mwezi 12 Mfungo 6 (Rabi-ul-Awwal).
Kwanza mwenzetu mmoja aliuliza kuhusu moto wa uajemi, asili yake na kama ulikuwa ukiwaka kila siku.
JIBU: Moto wa uajemi ulikuwa ukiwaka kila siku kwa madhumuni ya kuiabudu. Imeelezwa ndani ya (Kitabu cha) Taurati cha Mtume Musa kuwa moto huo utazimika mara tu Mtume wa mwisho (Swallallahu Alaihi Wasallam) atakapozaliwa, na ndivyo ilivyokuwa.
Pia kwa ufafanuzi tu, mfalme Abraha alijenga nyumba ya kuabudia sanamu huko sanamu ili watu waache kwenda Makkah kuabudu masanamu waliokuwepo ndani ya Al Kaaba.
Ifuatayo ni risala fupi kuhusu Mtukufu wa Daraja:-
Alla Azza wa Jalla amesema: “Hakika imekuja kwenu Nuru” (Quran 5:15). Vivyo hivyo kuna aya nyingi za Quran Tukufu zinazoelezea kuja kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam hpa duniani. Mmojawapo ya aya inasema: “Hatukupeleka wewe ila uwe ni Rahma kwa walimwengu” (Quran 21:107), pia “Hakika imekuja kwenu Nuru na uthibitisho iliyo wazi” (Quran 5:15), pia “Hakika amekuja Mtume miongoni mwenu” (Quran 9:128) na pia “Allah Ana Hisani juu ya Waumini kwa kumleta Mtume miongoni mwao” (Quran 3:164). Vile vile kuna aya nyingi za namna hii na hata kwenye Hadithi imeelezwa kuja kwa Mtume.
Kuelezea kuja kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, imetajwa kama: “Ewe Habibi Nimekutuma …”, “Mtume amekuja …” na “ameletwa …”. Mmoja akichunguza kwa makini maneno haya, ataamini kabisa kuwa mtu analetwa au kupelekwa ni yule alikuwepo sehemu moja mwanzoni. Hivyo itabidi tukubali kuwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam – Roho ya ulimwengu, tumaini la shida, Masiha kwa watu, Rahma kwa walimwengu – alikuwa sehemu fulani kabla ya kuletwa hapa duniani. Kabla ya kuletwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, hali ya dunia haikuwa nzuri. Kila kitu kilikuwa katika mchafuko. Ukafiri ulikuwa umeenea kila sehemu. Ulevi, kamari, riba na rushwa ilikuwa ni jambo la kawaida. Mitaani zinaa, ndoa ya jinsi moja, husuda, kusengenya, uadui na chuki zilienea. Ufidhuli, anyang’anyi na uuaji ilikuwa ndiyo maisha ya kila siku. Hapakuwepo hata herufu ya upendo, heshima na unyenyekevu miongoni mwa watu. Pia hapakuwepo na hifadhi ya maisha na mali. Jumuiya iliharibika sana kiasi cha mzazi kumzika hai binti wake. Katika wakati wa uharibifu kama huo, tumaini kwa wadhaifu, Rahma kutoka kwa Allah, Mtume wetu Mpendwa Swallallahu Alaihi Wasallam alizaliwa alfajiri ya Jumatatu, mwezi 12 Mfungo 6 (Rabi-ul-Awwal). Siku ya kuzaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, ulimwengu mzima uliingia mwangaza, ukafiri ulianza kuvurugika, moto wa uajemi ulizimika, upepo wa imani ulianza kuvuma, bendera ya Tauhid ilipandishwa, Nuru ilianza kuenea na wengi walioabudu miungu 360 (sanamu) sasa waligeuka katika ibada ya Allah Mmoja.
Kuna kila sababu ya Muislamu kuadhimisha siku hiyo Tukufu. Isitoshe Kiyam ya kumsalia Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam wakati Alfajiri inapoingia mwezi 12 (muda wa kuzaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam) na kisha dua inayoombwa muda huo, inakubalika moja kwa moja. Hivyo ni bora kusoma Qasida Burdai (YA RABBIBIL MUSTAFA BALLIGH MAQAASWIDANA …) usiku huo ili kupata faida kwani ni Qasida iliyokubalika mbele ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam.
Nawatakieni nyote pamoja na familia zenu Maulidi njema.
Maswali/ maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Kind Regards,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...