Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo. Tunaendelea na masimulizi yetu ya Maulidi na risala hapo chini inaelezea dalili za Maulidi kupitia Quran Tukufu na Hadithi.
DALILI NA UTHIBITISHO WA KUSHEREHEKEA NA KUADHIMISHA MAULIDI KUPITIA QURAN TUKUFU NA HADITHI. Allah Amesema ndani ya Quran Tukufu : “Sema (Ewe Mtume uwaambie) kwa Fadhila za Allah na Rahma Zake inatakiwa wafurahikie, hiyo ni bora kwao kuliko waliyoyakusanya”. (Sura Yunus: 58) Katika aya hii Allah Anatuagizia tufurahikie pindi tunapopata Fadhila na Rahma zake. Bila shaka, Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam ni Fadhila na Rahma kubwa kutoka kwa Allah. Allah Anatuambi : “Hatukukutuma (Ewe Mtume) ila uwe Rahma kwa walimwengu”. (Sura Ambiya: 107) Allah Amesema ndani ya Quran Tukufu : Ewe Mwenye Kusimulia habari za uficho (Ewe Mtume) Hakika sisi tumekutuma uwe Shahidi na Mbashiri na Mwonyaji. Na mwitaji kumwendea Allah kwa idhini Yake, na jua lenye kuangaza. Na wabashirie Waumini kwamba wana fadhila kubwa itokayo kwa Allah”. (Sura Ah-zaab: 45-47). Allah pia akasema : “….na uwakumbushe siku za Allah …” (Sura Ibrahim: 5) Wafasiri wanasema kuwa “siku za Allah” inamaanisha siku ambamo Allah Amewazawadia binadamu; kama vile kuongoka kwa Bani Israil na utumwa wa Firauni. Hivyo zawadi kubwa kuliko zote kutoka kwa Allah ni kuletwa (au kuzaliwa) kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam na hii inamaanisha kuwa Maulidi ya Mtume ni siku ya Allah; kwa hiyo ni lazima ikumbukwe/ itajwe. Pia Allah Anasema : “Hakika Allah Amewafanyia wema mkubwa Waumini kwa kuwaletea Mtume aliye miongoni mwao …” (Sura Aali Imran: 164). Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam mwenyewe alipoulizwa kuhusu kufunga (swaum) kwake kila siku ya Jumatatu, alijibu : “ni siku nilimozaliwa” (Al Muslim). Hii inaonyesha kuwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alifunga siku ya Jumatatu kumshukuru Allah kuzaliwa kwake. Pia Abu Jahal alipokufa, mmoja katika ndugu zake (Sayyidina Abbas RadwiyAllahu Anhu – Amii yake Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam) alimuota na kumuuliza hali yake baada ya kufa kwake. Abu Jahal alimjibu: ninaadhibiwa sana ila kila siku ya Jumatatu ninapunguziwa adhabu, pia ninaposikia kiuu basi hunyonya kidole changu cha shahada na husikia nafuu kidogo. Baba wa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam ni kaka yake Abu Jahal, hivyo siku alipozaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, Abu Jahal aliletewa taarifa na mtumwa wake (Thuwaibah) kuwa nyumbani kwa kaka yako amezaliwa mtoto wa kiume! Kwa furaha hiyo, Abu Jahal alimuashiria kwa kidole chake cha shahada kumuacha huru mtumwa wake huyo. Wanazuoni wanasema ikiwa kafiri mkubwa na adui mkubwa wa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam anapata nafuu katika adhabu yake kwa kufurahia tu kuzaliwa kwa mtoto wa kiume, je Muislamu akisherehekea Maulidi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam hatapata faida?? (Al Bukhari). Wanaelezea pia kuwa mwenye kusherehekea Maulidi kwa heshima na mapenzi ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, basi atazawadiwa na Allah. Wanaelezea pia kuwa mikusanyiko ya Maulidi huwa ya heshima na mapenzi kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam tu. Pia ieleweke kuwa shetani alilia mno alipozaliwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam na hivyo wanazuoni wanasema kuwa mwenye kuhuzunika na Maulidi, basi anamfuata shetani na huu si mwenendo wa Waislam.
Maswali/ maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Kind Regards,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...