Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo. Pia niwajulishe kuwa ninaanza likizo ya wiki 3 kuanzia kesho in sha Allah; ila darsa zetu zitaendelea kama kawaida kwani nitawaandikieni kutoka nyumbani.
Nashukuru sana hatimaye kupata maswali / maoni kutoka kwa ndugu zetu wawili (kama kawaida huwa siwataji). Nazo ni kami hivi:-
SWALI LA KWANZA:
Shukran Brother, lakini nina maoni na maswali kidogo.
Kwanza kabisa naomba nikiri kwamba mimi ni mchanga sana kwenye elimu hii ya dini, kama ni kufananisha basi elimu yangu haiwezi hata kufikia ukubwa wa punje moja ya mchanga kwenye mchanga wa dunia hii nzima, hivyo unisameha pale nitakapokosea lengo ni kupata elimu zaidi.
Risala yako imenifurahisha na kunipa mafunzo mengi ya matayarisho ya mfungo mtukufu unaokuja, nashukuru sana. Maoni yangu na maswali yangu yapo kwenye kipengele cha muandamo wa mwezi. Kama ulivyosema ni upuuzi mtupu kufikiri na kusema kwamba dunia nzima twaweza kufunga na kufungua pamoja.
MAONI
Nafikiri kwamba umetumia lugha kali sana kwa kuuita ni upuuzi mtupu kufikiri na kuamua kufunga kwa pamoja kwa dunia nzima. Uliposema ni upuuzi mtupu ina maana kwamba anyefanya kitendo cha kipuuzi na yeye ni mpuuzi. Kwangu naona kama kuna kundi ambalo litahisi linatukanwa kutokana na kauli hiyo. Hata Masahaba wamekuwa wakitofautiana lakini sijasikia mmoja akimuita mwenzake ni mpuuzi, hilo lilitosha kuvumiliana na kufanya kuwe na masikilizano. Sababu kama mtu akihii kutukanwa naamini hata baadaye ukifanya jitihada za kumuelimisha hatakusikiliza kwa kuchelea kutukanwa tena hivyo kukosa elimu kubwa ambayo ungempa. Sisi sote tuko kwenye jitihada za kuijua dini hivyo uelewa unatofautiana tukitumia lugha nzuri kufahamishana tutafikia sehemu tutakuwa kitu kimoja. Nilipata kusikia kisa kimoja kuna sahiba ambeye yeye alikuwahakunuti wakati wa sala ya Alfajir, basi siku moja alipoetaka kukunuti kwa vile alikuwa na shida na antaka kukunuti katika sala yake ya Subhi alienda kusali kwenye msikiti ambao wao huwa wanakunuti lakini alipofika na Yule sahaba mwenzake ambaye alikuwa imamu alipomuona akaamua asikunuti kwa siku hiyo ili asimkwaze mwenzake. Baada ya sala alipoulizwa kwa nini hakukunuti akasema alichelea kumkwaza mgeni aliyekuja Sali nao na mgeni akaeleza kwamba yeye alikuja ili apate kunuti, hii inaonyesha jinsi gani masahaba waliweza kuvumiliana na kutumia mbinu ili kutomkwaza mtu mwingine. Naamini na sisi tukitumia njia hii tutafika tulipokusudia
NB: kama nilvyotahadharisha tokea mwanzo elimu yangu ni ndogo naomba mwongozo nilipokosea.
Shukran sana, in sha Allah nitazingatia.
SWALI
Je tunatakiwa tutumie mipaka gani kujua sisi tunafunga na kundi gani? Je ni mipaka hii iliyowekwa na binadamu au kuna mipaka mingine tunayotumia? Na kama tulivyoelekezwa tunapohitilafiana turudi kwenye kitabu chetu kitukufu(Qur an) pamoja na sunnah za mtume SAW. Je kuna Aya au Hadith inayoongelea tutumie mipaka iliyowekwa na mwanadamu. Kama ni suala la umbali tunapoongelea muda wa kuchomoza na kuzama kwa jua, muda ambao jua huchomoza Dar es salaam na Saudia hauna tofauti sana kama ukilinganisha muda jua linapochomza au kuzama kigoma. Hivyo basi ilipendeza zaidi sisi na Saudia kufunga siku moja na Kigoma wafunge siku ya pili. Inakuwaje Rwanda na Burundi wafunge lakini Kigoma wasubiri mpaka Dar es salaam watangaze mwezi umeandama, je tunatumia umbali wa eneo au mipaka iliyowekwa na binadamu?
Nitashukuru nikielimishwa zaidi, kwani Allah na Mtume(SAW) wake ndio wenye kujua zaidi.
In sha Allah nitaifuatilia na kuwajibu haraka iwezekanavyo.
SWALI LA PILI
Me swali langu liko hivi,wakati wa mtume watu walikuwa wakiwa na matatizo wanaenda kwa bwana mtume na kuwaambia ewe muhammad niombee kwa mola wako nina shida fulani,na bwana mtume alikuwa akiwaombea na watu wanafanikiwa.sasa hivi kuna masharifu kuna masheikh ambao wanawaombeaga watu,mimi kitu kimoja kinanisumbua mtu anaenda kwa sheikh anamwambia dua yake inabid kuchinja mbuzi au kuku je hiyo ni sawa? na hakuna shirk ndani yake,ni kweli kuna watu wana kalima ya kuwaombea watu dua?
Shirk hupatikana pale kiumbe anaposhirikishwa na Allah katika ibada. Mfano: Unamuabudu Fulani (astaghfirullah), tayari ni shirk.
Swali lako linagusa kitu kinaitwa KUTAWASSUL (kuomba kupitia kwa ….). Kuna uthibitisho wa kutosha ndani ya Quran na Hadithi kuhusu hilo. Mfano baada ya Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam kuiaga dunia hii, mji wa Madina ulikumbwa na ukame ajabu na hakuna mvua kwa siku kadhaa. Masahaba walimkalisha Amii yake Mtume, Sayyidina Abbas, juu ya mimbar na kumuomba Allah kupitia kwa Amii wa Mtume kuwa inyeshe mvua, mara ikanyesha. Kuhusu kuchinja, hiyo ni sadaka na inategemea na tatizo mtu alilonalo.
Kama bado hilakaa vizuri basi naomba usisite kuuliza tena.
Swali lapili linahusu mwezi mtukufu wa ramadhani,mwaka jana kuna siku ambazo kinadada wanaziacha kwa sababu ya siku zao au uja uzito au ugonjwa ,baada ya ramadhani kuisha haikuwezekana kulipa kutokana na hali kiafya,na sasa ramadhani inaingia sijalipa bado,ramadhani ikija hizo siku zinalipika tena.
Saumu yoyote ya Ramadhan (ambayo ni faradhi) ni lazima kulipwa haraka iwezekanavyo. Saumu yoyote ya Sunnah haikubaliki kama faradhi bado kulipwa. Kwa hali iliyoelezwa hapo juu, jitahidi baada ya Ramadhani hii ulipe haraka iwezekanavyo. Kumbuka ya kuwa sita za Mfungo Mosi hazitakubalika kama za Ramadhani bado kulipwa.
Narudia kutoa shukurani kwa kuuliza au kutoa maoni na bado naendelea kusisitiza Maswali / maoni mengine pia.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...