Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo na mko tayari kabisa kumpokea mgeni wetu mtukufu – asiyehitaji kukagua gwaride wala kuwanyanyasa ama kuwatesa wenyeji wake!! Ni mgeni anayetaka manufaa yetu tu, atakuja kutufurahisha na zawadi kemkem zisizo na mfano ila atatuaga tukitoa machozi!!
Karibu mgeni wetu RAMADHAN KAREEM! (kuanzia Jumatano in sha Allah)
Ifuatayo ni sehemu ya mwanzo ya risalah kuhusu fadhila na faida za mwezi Ramadhan.
AYA: YAA AYYUHALLADHINA AMANU KUTIBA ALAIKUMUS SIYAAMA KAMA KUTIBA ALAL LADHINA MIN QABLIKUM LA-ALLAKUM TATTAKUN.
Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam, aya hapo juu ya 183 ya Sura Al Baqarah inayozungumzia saumu na ndiyo itakuwa mada yetu.
Tafsiri ya aya:
Enyi mloamini mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa wale walikutangulieni, ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu.
Tumepata kujua kupitia aya hii kuwa Allah amefaradhisha kufunga. Ikumbukwe kuwa ummah zilizotangulia pia walifaradhishiwa kufunga. Mfano: Mtume Adam Alaihissalaam alifunga tarehe 13, 14 na 15 ya kila mwezi. Mtume Daud Alaihissalaam alifunga siku moja na siku moja huacha na hiyo ilikuwa maisha yake yote. Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam amesema kuwa Allah alizipenda sana funga za Mtume Daud.
Allah amefaradhisha saumu 30 kwa mwaka mzima, na kama mwezi ukiandama 29 basi saumu zitakuwa 29. Waislamu duniani kote wamezusha fitna moja kubwa sana. Wanadai eti itakuwa bora zaidi Waislamu wote wafunge siku moja, washerehekee idi siku moja; baadhi hadi wakadai eti mwezi ukiandama Saudia basi Waislamu duniani kote wafunge. Huu ni upuuzi mtupu. Kuna uthibitisho tosha kupitia Quran na Hadithi kuwa kama mwezi haukuandama wa 29 basi kamilisheni idadi ya 30. Vile vile imethibitika mara kadhaa kuwa Saudia wanatangaza kufunga au idi pasipo na muandamo wa mwezi.
Faradhi ya kufunga na thawabu zake.
Hadithi iliyopokelewa na Salman Farsi; amesema kuwa zilikuwa siku za mwisho wa mwezi Shaabaan, Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alituambia tusubiri kuna nasaha anataka kutupatia.
Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alianza kusema kuwa mwezi unaotarajiwa ni tukufu sana. Allah amefaradhisha saumu za mwezi wa Ramadhani kwa Waislamu, ameweka thawabu katika ibada ya usiku, ina usiku mmoja ambao ibada yake ni bora kuliko ile ya miezi 1,000 nayo ni Laylatul Qadri.
Mwenye kutenda amali njema ndani ya mwezi huu ili kumkaribia Allah, basi thawabu zake ni sawa na zile za faradhi; maana yake mwenye kutenda sunnah katika mwezi wa Ramadhani basi Allah anamuandikia thawabu sawa na kutenda faradhi. Ikazuka swali ikiwa Sunnah ina thawabu ya faradhi, je faradhi thawabu yake itakuaje? Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam akasema mwenye kutenda faradhi basi Allah humuandikia thawabu sawa na kutenda faradhi 70.
Katika mwezi wa Ramadhani, Allah huzidisha riziki za Waislamu, wasaidieni wasiojiweza katika mwezi huu, mwenye kumfuturisha Musilamu ndugu yake basi ana fadhila 3 – (1) Allah humsamehe madhambi yake (2) Allah humuacha huru na moto wa jahannam (3) Allah humjaalia thawabu ya saumu 1 ya ziada bila ya kumpunguzia thawabu aliyefuturishwa.
Saumu zimefaradhishwa mwaka wa 2 baada ya hijrah. Hali za Waislamu ilikuwa duni sana. Vita vya Badr vilitokea mwezi wa Ramadhani, makafiri waliotekwa walikabidhiwa Masahaba pamoja na hali zao duni. Masahaba walikula tende lakini waliwapikia chakula wageni wao watekwa; kitendo hicho kiliwavutia sana watekwa hao na baadhi yao walisilimu. Masahaba walimuuliza Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam kuwa hawana uwezo wa kumfuturisha hadi kushiba, je sisi tutakosa thawabu hizo? Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam akajibu mwenye kumfuturisha Muislamu mwenzake japo tende 1 au glasi tu ya maji, basi atapata thawabu zilizotajwa.
Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam akaendelea kusema kuwa mkithirishe mambo manne mwezi wa Ramadhani: (1) kusoma Kalima (2) kuleta istighfar (3) kuomba Pepo (4) kuomba huru na moto wa jahannam.
Wapunguzieni mzigo wafanyakazi wenu katika mwezi wa Ramadhani, maana yake kupunguza muda wa kazi.
Mwenye kumfuturisha Muislamu mwenzake japo kwa tende 1 au glasi tu ya maji, basi Allah atamnywesha maji matukufu ya Bwawa la Kauthar na hatashikwa na kiuu hadi kuingia Peponi.
Maswali / maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...