Assalaamu alaikum,
Natumai hamjambo na mnaendelea na ibada tukufu ya swaum. Ifuatayo ni sehemu ya pili ya risala yetu.
AYA: YAA AYYUHALLADHINA AMANU KUTIBA ALAIKUMUS SIYAAMA KAMA KUTIBA ALAL LADHINA MIN QABLIKUM LA-ALLAKUM TATTAKUN.
Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi Wasallam, aya hapo juu ya 183 ya Sura Al Baqarah inayozungumzia saumu na ndiyo itakuwa mada yetu.
Tafsiri ya aya:
Enyi mloamini mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa wale walikutangulieni, ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu.
Hadithi tuliyosimulia Ijumaa iliyopita, ina maelezo zaidi, na tutazichambua kwa ufupi.
Tumefaradhishiwa saumu. Ila kama kuna mgonjwa au msafiri au mwanamke katika siku za hedhi zake, hao wameruhusiwa kutofunga siku hizo. Baada ya kukamilisha idadi ya 29 au 30, basi wanatakiwa wafunge siku walizoacha. Ila hawaruhusiwi kula hadharani. Pia mtu mzee asiye na nguvu na wala hatarajii kupona, itambidi atoe fidia badala ya saumu zake. Lau kama atapata nguvu, basi ni bora kwake kufunga na si kutoa fidia.
Qiyam / ibada ya usiku imefanywa kuwa ni ya thawabu. Ibada ya usiku ni raka 20 za Tarawih, nayo ni Sunnah iliyosisitizwa kwa wanaume na wanawake. Ni bora kwa kina mama kusali nyumbani. Hadi mwanzoni mwa Ukhalifa wa Sayyidina Umar, Masahaba walisali Tarawih peke yao. Ndipo Sayyidina Umar aliwakusanya nyuma ya imam mmoja nae ni Ubay bin Ka’ab, ambae aliwasalisha rakaa 20. Baadhi ya watu wanadai Tarawih ni raka 8. Ikumbukwe raka 8 ni tahajjud na si Tarawih.
Pia kiakili naomba tuzingatie; ikiwa Tarawih ni rakaa 8 na sisi tunasali rakaa 20, siku ya Kiyama Allah Akituuliza kwa nini umezidisha rakaa 12, basi japo tutaweza kumuomba kwa Rehema zake atujaalie thawabu ya ziada kwa hizo rakaa 12. Lakini je wanaosali rakaa 8 na Allah akiwauliza kuwa Tarawih ni 20 kwa nini mkasali 8 tu, hebu jiulize hizo rakaa 12 watazitoa wapi!! Naomba tusipumbazike na wanaodai kuwa eti ni rakaa 8 tu!! Laa hasha! Tarawih ni rakaa 20.
Mna usiku mmoja ambayo ibada yake ni bora kuliko ibada ya miezi 1,000. Miezi 1,000 ni miaka 83 na ieleweke kuwa umri wa ummah huu ni karibia miaka 60.
Imeelezwa kuwapunguzia mzigo wafanyakazi wenu mwezi huu. Mtume amesema kuwa mwenye kumpunguzia mzigo mfanyakazi wake, basi Allah atampunguzia mzigo siku ya Qiyama.
Mtume ameeleza kuwa siku zake 10 za mwanzo Allah anawarehemu waja wake, 10 za kati Allah anawasamehe waja wake na 10 za mwisho ni kuongoka na moto wa jahannam.
Imeelezwa kukithirisha mambo manne: Kalima, istighfar, kuomba Pepo na kuomba huru na moto wa jahannam.
Mwenye kumfuturisha Muislamu mwenzake, hujaaliwa thawabu ya saumu moja mwenye kumnywesha maji, basi Allah atamjaalia maji ya Kauthar na hatashikwa na kiuu hadi kuingia Peponi.
Pia zingatia kusoma dua zifuatazo:-
1) LAA ILAHA ILLALLAHUL HAYYUL QAYYUMUL QAA-IMU ALAA KULLI NAFSIM BIMAA KASABAT (mara 7 baada ya kula daku; thawabu kwa kila nyota ya mbinguni)
2) ALLAHUMMAR HAMNA YAA AR HAMAR RAAHIMIN (soma kwa wingi katika siku hizi 10 za mwanzo)
3) LAA ILAHA ILLALLAH ALLAHUMMA NASTAGHFIRUKA WA NAS-ALUKAL JANNATA MA-AL ABRAARI YAA AZIZU YAA GHAFFAARI (pendelea kusoma kila mara mwezi mzima)
Maswali / maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...