Natumai hamjambo. Ijumaa Kareem.
Tunaendelea na risala juu ya maisha ya Mtume Ibrahim Alaihissalaam.
AYA: FALAMMA BALAGHU MA-‘AHUS SA-‘AYA, QAALA YA BUNAYYA INNI ARAA FIL MANAMI ANNI ADH BAHUKA FANZUR MAA DHAA TARAA. QAALA YA ABATI-F-‘AL MAA TU-UMARU SATAJIDUNI INSHA ALLAHU MINAS SWABIRIN.
Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi wasallam, hapo juu ni aya ya 102 ya Sura SWAAF-FAAT (37:102), inayozungumzia kisa cha kuchinja
Mtume Ibrahim baada ya kuwaacha mkewe na mwanae kwenye jangwa, alikuwa akiwapitia kuwajulia hali. Mwanzoni alikuwa akiwajulia hali akiwa juu ya mnyama na kisha huondoka bila ya kushuka. Baadae alianza kujipumzisha nao kwa siku mbili au tatu hivi. Ni katika safari yake hizo alipojipumzisha, usiku alioteshwa akisikia sauti ikimwambia atoe katika njia ya Allah kile anachokipenda mno. Asubuhi yake alitoa mali katika njia ya Allah. Usiku wa pili pia alioteshwa kama usiku uliopita na kisha asubuhi yake alitoa mali. Usiku wa tatu ndipo alioteshwa akimchinja mwanae na hapo ndipo alielewa kuwa ni amri ya Allah. Asubuhi yake alimwambia mkewe kuwa amuogeshe mwanae na amvalishe mavazi mazuri kwani wanaenda kuchinja.
Shetani daima havumilii kuona kuwa hukumu ya Allah inatekelezwa. Hivyo kwanza alimjia mama Hajirah huku akiwa amejivalia kama shehe. Akamwambia hivi unafahamu mumeo ameelekea wapi? Mama akamjibu wameenda kuchinja. Shetani akamwambia ameenda kumchinja mwanao. Mama akamwambia kuwa hivi kuna mzazi anaemchinja mwanae? Shetani akasema swali lako ni sahihi, ila mumeo anadai amehukumiwa na Allah. Kusikia hivyo tu mama Hajirah akamwambia inaelekea wewe ni shetani, kama ni amri ya Allah basi ni bahati yetu hiyo na Allah Aikubali utekelezaji wetu tu. Baada ya hapo alimuendea Mtume Ibrahim na kumdanganya kuwa eti hiyo ni ndoto tu na hivyo asiitilie maanani, lakini Mtume Ibrahim nae alimkimbiza. Kisha akaanza kumshawishi Mtume Ismail kuwa eti baba yake anaenda kumchinja kwani anadai amehukumiwa na Allah. Mtume Ismail alipomkimbiza, ndipo shetani akasimama katikati ya njia huko Mina’a. Akasema hatomruhusu Mtume Ibrahim kutekeleza amri ya Allah. Allah alimuambia Mtume Ibrahim achukue jiwe 7, asome Takbir na ampige shetani. Ni kitendo ambacho leo mahujaji wanakitekeleza. Alifanya hivyo mara 3 na kisha wakafika sehemu ya kuchinja kwenye uwanja wa Mina’a.
Kwanza kabisa Mtume Ibrahim alimueleza mwanae, kama aya inavyoeleza:
Tafsiri: Basi (Mtume Ismail) alipofika umri wa kwenda na kurudi pamoja nae, Mtume Ibrahim akamwambia: “ewe mwanangu! Hakika nimeona usingizini kuwa ninakuchinja, je wewe unaonaje? Ismail akamjibu: ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa, utanikuta mimi, kwa uwezo wa Allah, katika wanaosubiri.
Hapo ndipo Mtume Ibrahim akamumbatia mwanae, ila Mtume Ismail alimpa masharti baba yake kabla ya kuchinjwa. Baadhi ya masharti ni kuwa Mtume Ibrahim afunge kitambaa cheusi machoni mwake ili asiweze kumuona anamchinja mwanae, Mtume Ismail afungwe kamba miguu na mikono yake ili asitapetape, aanza kumchinja shingoni ili uso wake asiuone. Mtume Ibrahim alifanya hivyo ndipo alianza kumchinja mwanae.
Mtume Ibrahim alianza kutembeza kisu lakini kisu ikashindwa kukata na ndipo Allah Alimuamrisha Jibrael kuacha makazi yake huko Sidrah mara moja, amchukue ndama wa Peponi na amlaze sehemu alipolazwa Mtume Ismail. Jibrael alitekeleza amri hiyo kwa kasi isiyo ya kawaida na kama Allah Alivyosema ndani ya Quran:
AYA: WANADAINAHU AN YA IBRAHIM, QAD SWADDAQTAR RU-UYA. Na tulimuita: Ewe Ibrahim! Umetimiza ndoto, hakika hivi ndivyo tunawalipa watendao mema. (SWAAF-FAAT – 37: 104-105)
Jibrail alikuja na ndama akisoma ALLAHU AKBAR ALLAHU AKBAR, Mtume Ibrahim aliposikia nae akasoma LAA ILAHA ILLALLAHU WALLAHU AKBAR, na Mtume Ismail akasoma ALLAHU AKBAR WALILLAHIL HAMD. Hivyo Mtume Ibrahim akamchinja ndama wa Peponi badala ya mwanae Mtume Ismail.
SWALI: Kuna ndugu yetu ameuliza: katika kuchinja mnaweza kuungana kwa idadi maalum au idadi yoyote ile?
JIBU: Kwa mbuzi ni mtu mmoja kwa mbuzi, ila kwa ng’ombe ni watu saba kwa ng’ombe mmoja.
Maswali / maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI
0 comments:
Post a Comment
Enter your Comment here...