Ads 468x60px

Mar 10, 2025

RAMADHAN KAREEM - PT 3 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo na mnaendelea na ibada za Mwezi Mtukufu. Tunaendelea na risala yetu. 

 

 

 Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad , hapo juu ni aya ya 10 na 11 ya Sura As-Swaaf kutoka Quran inayozungumzia jihad na ndiyo itakuwa mada yetu.

 

Tunaendelea na mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mwezi ambamo mambo kadhaa yamedhihirika. Ni katika mwezi huu saumu ikafaradhishwa, qiyam ya usiku yaani sala ya tarawih ikawekwa ni jambo la thawabu, ni mwezi wa kuomba dua na ni mwezi ambamo dua inakubalika. Pia ni mwezi ambamo mna usiku wa Lailatul Qadri. Fadhila nyingine ni kuwa Quran imetelemshwa katika mwezi huu.

Wafasiri na wanazuoni wakuu wanaelezea kuwa vitabu vyote vya mbinguni vimeteleshwa katika mwezi huu.

 

Ni katika mwezi huu katika maeneo ya Badri, vita kati ya Waislamu na makafiri, iitwayo vita vya Badri, ilitokea ambayo ilidhihirisha ujasiri wa Uislamu. Makafiri walidhalilika mno na hawakutegemea kabisa. Hivyo leo tutazungumzia kuhusu vita vya Badri ili kujipatia thawabu za kuwakumbuka Masahaba mashujaa waliojitolea kwa hali na mali kuitetea Uislamu.

 

Tafsiri ya aya: Enyi mloamini, je Nisiwaonyeshe biashara itakayowaokoa na adhabu kali? Muaminini Allah na Mtume Wake, na piganeni jihad katika njia ya Allah, kwa mali yenu na nafsi zenu, haya ni bora kwenu ikiwa mnafahamu. (SURA: AS-SWAFF: 10-11)

 

Biashara ni jambo ambalo inampatia mtu faida. Hapa Allah Anazungumzia kuleta imani juu ya Allah na Mtume Wake, kusoma kalima, ndipo itamletea mtu faida; vinginevyo hatapata faida yoyote. Kisha Allah akaagiza jihad katika njia Yake kwa mali na nafsi zetu; na hii akaitaja kuwa ni bora kwetu.

 

Hivi sasa Waisalmu wanadhalilika ulimwenguni ni kwa sababu ya kuacha jihad. Pili mali na pesa imewafanya watu kuwa waoga. Tatu jihad huzidisha hadhi ya Uislamu. Uislamu ni dini ya amani, lakini pindi inapoandamwa kutaka kuangamizwa, basi ni vyema ikahifadhiwa kwa jihad. Anaeuawa katika jihad ni shahidi. Pia anaejeruhiwa katika jihad, basi siku ya kiyama damu itatoa ushahidi wa kunukia kama zafarani. Shahidi hataogeshwa bali atakafiniwa katika nguo zenye damu, atasaliwa jeneza na kuzikwa. Siku ya kiyama atafufuliwa na nguo zake za damu.

 

Hadithi: Mtume amesema kuwa mtu mwenye macho aina mbili hataingia motoni. Moja: ni mwenye kutokwa na machozi katika hofu ya Allah na PILI macho yaliyokesha wakati wa jihadi ikichunga uvamizi wa adui.

Hadithi: Mtu huyu hataingia motoni ambae miguu yake ikapatwa na vumbi katika njia ya Allah.

 

 

Katika vita vya Badri, Waislamu walikuwa 313 tu wakiwa na farasi 17 tu na mikuki kama 8 na pia hawakujianadaa kabisa kupigana. Makafiri walikuwa kati ya 900 na 1,000 na kila mmoja alikuwa na farasi au ngamia na vifaa vyote na walijiandaa kikamilifu. Makafiri walikuja na dhamira ya kuwadhalilisha Waislamu. Masahaba walimtayarishia Mtume banda la kukaa na kutoa amri. Iliponadiwa nani atakaemlinda Mtume , AbuBakr Siddiq ndiye aliyejitokeza.

 

Makafiri 70 waliuawa katika vita wakati Masahaba 14 tu wakawa mashahidi. Usiku wa kuamkia siku ya vita, Mtume alipotembelea uwanja wa vita, aliweka alama kuwa kafiri Fulani atakufa hapa na Fulani hapa, na ndivyo ikawa.

 

Wakati wa vita, walikuja watoto wawili kwa AbdulRahman bin Auf na kumwambia waonyeshwe aliko Abu Jahal ili wakamuue kwani anamtukana sana Mtume . Walipoonyeshwa, mmoja alimpiga panga la nguvu hadi mguu kuvunjika. Jeuri lake likawa pale tu kwani kabla ya kufa alisikitika mno kupigwa na watoto wadogo badala ya jemedari kama yeye.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

Mar 4, 2025

RAMADHAN KAREEM - PT 2 [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo na mnaendelea na ibada za Mwezi Mtukufu. Tunaendelea na risala yetu.

Baada ya Kumshukuru Allah na kumtakia Rehma Mtume Muhammad , imesomwa aya ya Quran inayozungumzia saumu na ndiyo itakuwa mada yetu.

 

Tafsiri ya aya:

Enyi mloamini mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa wale walikutangulieni, ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu.

Hadithi tuliyosimulia Ijumaa iliyopita, ina maelezo zaidi, na tutazichambua kwa ufupi.

 

Tumefaradhishiwa saumu. Ila kama kuna mgonjwa au msafiri au mwanamke katika siku za hedhi zake, hao wameruhusiwa kutofunga siku hizo. Baada ya kukamilisha idadi ya 29 au 30, basi wanatakiwa wafunge siku walizoacha. Ila hawaruhusiwi kula hadharani. Pia mtu mzee asiye na nguvu na wala hatarajii kupona, itambidi atoe fidia badala ya saumu zake. Lau kama atapata nguvu, basi ni bora kwake kufunga na si kutoa fidia.

 

Qiyam / ibada ya usiku imefanywa kuwa ni ya thawabu. Ibada ya usiku ni raka 20 za Tarawih, nayo ni Sunnah iliyosisitizwa kwa wanaume na wanawake. Ni bora kwa kina mama kusali nyumbani. Hadi mwanzoni mwa Ukhalifa wa Sayyidina Umar, Masahaba walisali Tarawih peke yao. Ndipo Sayyidina Umar aliwakusanya nyuma ya imam mmoja nae ni Ubay bin Ka'ab, ambae aliwasalisha rakaa 20. Baadhi ya watu wanadai Tarawih ni raka 8. Ikumbukwe raka 8 ni tahajjud na si Tarawih.

Pia kiakili naomba tuzingatie; ikiwa Tarawih ni rakaa 8 na sisi tunasali rakaa 20, siku ya Kiyama Allah Akituuliza kwa nini umezidisha rakaa 12, basi japo tutaweza kumuomba kwa Rehema zake atujaalie thawabu ya ziada kwa hizo rakaa 12. Lakini je wanaosali rakaa 8 na Allah akiwauliza kuwa Tarawih ni 20 kwa nini mkasali 8 tu, hebu jiulize hizo rakaa 12 watazitoa wapi!! Naomba tusipumbazike na wanaodai kuwa eti ni rakaa 8 tu!! Laa hasha! Tarawih ni rakaa 20.

 

Mna usiku mmoja ambayo ibada yake ni bora kuliko ibada ya miezi 1,000. Miezi 1,000 ni miaka 83 na ieleweke kuwa umri wa ummah huu ni karibia miaka 60.

 

Imeelezwa kuwapunguzia mzigo wafanyakazi wenu mwezi huu. Mtume amesema kuwa mwenye kumpunguzia mzigo mfanyakazi wake, basi Allah atampunguzia mzigo siku ya Qiyama.

 

Mtume ameeleza kuwa siku zake 10 za mwanzo Allah anawarehemu waja wake, 10 za kati Allah anawasamehe waja wake na 10 za mwisho ni kuongoka na moto wa jahannam.

Imeelezwa kukithirisha mambo manne: Kalima, istighfar, kuomba Pepo na kuomba huru na moto wa jahannam.

Mwenye kumfuturisha Muislamu mwenzake, hujaaliwa thawabu ya saumu moja mwenye kumnywesha maji, basi Allah atamjaalia maji ya Kauthar na hatashikwa na kiuu hadi kuingia Peponi.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

Feb 27, 2025

AHLAN WA SAHLAN YAA SHAHRI RAMADHAN [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo.

 

Mwezi mtukufu ndiyo umeingiza mguu mmoja kwetu na in sha Allah, tutakuwa ndani ya swaum. Allah Atujaalie wepesi, afya njema na kibwa zaidi Atukubalie ibada zetu, ameen.

 

Ifuatayo ni utangulizi wa risala za mwezi Ramadhan. 

 

Baadhi ya matukio (tarehe) muhimu katika mwezi wa Ramadhani:

Tarehe 1: Kuzaliwa kwa Sheikh Sayyid AbdulQadir Jilani

Tarehe 3: Fatima binti Rasul RadwiyAllahu Anha kuiaga dunia

Tarehe 10: Mama Khadija RadwiyAllahu Anha kuiaga dunia.

Mama aliyekuwa tajiri na mfanyabiashara maarufu wa Makkah, aliolewa na Mtume akiwa na umri wa miaka 40 wakati umri wa Mtume ulikuwa miaka 25. Na ilitokana na uaminifu wa Mtume katika safari zake za biashara ya Mama Khadija. Mtumwa wake alimsimulia kuwa kila Mtume alipotembea basi kuwa wingu nayo ilitembea nae ikimpa kivuli. Na pia katika safari yake ya kwanza tu, wakati wengine walipata hasara katika biashara zao, Mtume alimletea faida maradufu Mama Khadija. Hicho kilimvutia sana hadi kupeleka posa la kutaka kuolewa na Mtume.

Baada ya kuolewa, Mama Khadija alisalimisha mali yake yote kwa Mtume ili itumike katika kuinusuru Uislamu.

 

Tarehe 17: Vita vya Badri (kisa kitafuata katika risala ya baadae) na Mama Aisha RadwiyAllahu Anha kuiaga dunia.

 

Mama Aisha, ambae ni binti wa Sayyidina AbuBakr Siddiq RadwiyAllahu Anhu, alikuwa mjuzi sana katika mambo ya dini na anamfuatia Bwana Abu Huraira katika kupokea riwaya kwa wingi Hadithi kutoka kwa Mtume.

 

Tarehe 21: Kuuawa shahidi kwa Sayyidina Ali RadwiyAllahu Anhu.

 

Usiku wa 21, 23, 25, 27 na 29 ni Laylatul Qadr.

 

Katika 10 za mwanzo, tukithirishe sana kutamka ALLAHUMMAR HAMNA YAA ARHAMAR RAAHIMIN.

 

Katika 10 za kati, tukithirishe sana kutamka ALLAHUMMA RABBANAGH FIRLANA DHUNUBANA YAA RABBAL AALAMIN.

 

Na katika 10 za mwisho: ALLAHUMMA QINA ADHABANNAARI WA-ADKHILNAL JANNATA MA-AL ABRAARI YAA AZIZU YAA GHAFFAAR.

 

RAMADHAN KAREEM!

Feb 8, 2025

NISF SHA'ABAAN [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

Natumai hamjambo.

Katika mwezi huu wa Sha’abaan mna usiku, ambao ni mwezi 14 kuamkia 15, ambamo mahesabu ya binadamu kwa mwaka uliopita hufungwa na vile vile matukio ya mwaka unaokuja huandikwa. Hivyo ni vyema tukawa katika ibada ili daftari letu kwa mwaka unaoisha ufungwe kwa ibada na ule wa mwaka unaoanza nao ufunguliwe kwa ibada.

Mmojawapo ya ibada iliyopendekezwa ni kusoma Sura Yasin mara 3 pamoja na Dua ya Nisf Sha’abaan baada ya sala ya Maghrib.

Pia Saum ya Nisf Sha'baan nayo ina fadhila zake.

Allah Atujaalie wepesi.

Jazak Allah.

Jan 30, 2025

SHA'ABAAN [Kiswahili]

Assalaamu alaikum,

 

Natumai hamjambo.

 

Mwezi wa nane katika Kalenda ya Kiislamu ni Sha'abaan. Utukufu wa mwezi huo juu ya miezi mingine ni kama ule wa Mtume juu ya Mitume wengine.

 

BAADHI YA TAREHE MUHIMU:

 

Qiblah ilibadilishwa kutoka Baytul Maqdis na kuwa Al Kaaba.

 

Imam Abu Hanifa, mmoja kati ya Maimamu wanne, kuiaga dunia hii tarehe 2.

 

Imam Husein RadwiyAllahu kuzaliwa tarehe 6.

 

Usiku wa kuwa huru na moto wa Jahannam (au kasimatu rizki) tarehe 15.

 

KUBADILIKA KWA QIBLAH:

 

Baytul Maqdis (Msikiti wa Aqsa) ulikuwa ndiyo Qiblah ya mwanzo ya Waislamu. Karibu Mitume wote waluielekea katika sala zao. Mtume alitamani sana kuelekea Al Kaaba tangu mwanzo tu.

 

Kila Mtume aliposali akielekea Baytul Maqdis, Mayahudi hukasirika sana na hata husema "inakuaje Mtume wenu anawaamrisheni kutenda kinyume na Mayahudi na inapokuja swala ya ibada basi anauelekea mji wetu (Jerusalem)?" Mtume hakujisikia kabisa vizuri kwa maneno hayo ya Mayahudi na alitamani sana kuelekea Al Kaabah.

Sub-Hanallah! Mara moja Allah Akatelemsha aya inayoelezea: "Tunashuhudia ukiinua uso wako mara kwa mara mbinguni. Basi tutakuelekeza upande wa Qiblah uiridhiayo wewe. Elekea Msikiti wa Haraam (Al Kaaba) sasa hivi, na enyi Waislamu! Elekeze nyuso zenu huko pia, popote mlipo .." (Quran Tukufu 2:144). Zingatieni watukufu Waislamu kuwa badiliko la Qiblah limetokea kwa sababu tu ya kumridhisha Mtume . Kuanzia hapo qiblah yetu ni Al Kaaba huko Makkah.

 

IMAM ABU HANIFA:

 

Jina lake hasa ni Nooman bin Thabit bin Zuta bin Mah. Alizaliwa katika mji wa Kufa, Iraq, mwaka wa 80 Hijria. Alikuwa katika zama tukufu wa Tabi'in (wale waliowafuata Masahaba).

 

Amepokea Abu Huraira RadwiyAllahu Anhu kuwa Mtume amesema kuwa : Katika ummah wangu atakuja mtu ataitwa Abu Hanifa. Siku ya Qiyama yeye (Abu Hanifa) ndiye atakuwa taa ya ummah wangu. Hadithi nyingine imeeleza kuwa "katika kila karne idadi Fulani ya ummah wangu utakuwa na daraja ya juu; Abu Hanifa atakuwa na daraja ya juu zaidi katika zama zake".

 

Miongoni mwa Masahaba aliokutana nao ni Sayyiduna Anas bin Maalik, Sayyiduna Sahl bin Saad na Sayyiduna Abul Tufail Amir bin Wathila RadwiyAllahu Anhum. Imam Abu Hanifa alipata elimu ya dini kupitia baadhi ya Masahaba na wanazuoni wapatao kama 4,000. Baadhi ya Masahaba ni Sayyiduna Hammad Basri, Sayyiduna Ata bin Abi Rabah, Sayyiduna Ikramah, Sayyiduna Imam Baaqir, Sayyiduna Imam Jafar Saadiq, Sayyiduna Abu Ali, Sayyiduna Abu Hurayrah, Sayyiduna Abdullah Ibn Umar, Sayyiduna Aqabah bin Umar, Sayyiduna Safwaan, Sayiduna Jabir na Sayyiduna Abu Qatadah RadwiyAllahu Anhum.

 

Imam Abu Hanifa alikuwa mfanya biashara na kila Ijumaa alikuwa akitoa sarafu 20 za dhahabu kwa wasiojiweza kama sadaka. Kwa muda wa miaka 40 Imam alisali sala ya Alfajiri kwa udhu ule ule wa sala ya Ishai (kwa maana usiku kucha alikuwa katika ibada bila ya kulala). Imam alihiji mara 55. Alihitimisha Quran Tukufu kila siku kimoja na usiku kimoja. Pia alikuwa akihitimisha Quran Tukufu katika rakaa moja ama mbili. Alikuwa mcha Mungu sana kiasi cha kufunga mwaka mzima (isipokuwa siku zile 5 zilizokatazwa) kwa muda wa miaka 30. Mahala alipofariki, alisoma Quran Tukufu 7,000.

WATUKUFU WAISLAMU TUPO JAMANI!!!

Mwezi Sha'abaan mwaka 150 Hijria, Imam aliiaga dunia hii huko Iraq akiwa katika hali ya sala, akiwa na umri wa miaka 70. Jeneza lake lilisaliwa mara 6 na kila mara waumini wapatao 50,000 walihudhuria na wengine walikuja kumuombea kwenye kaburi lake kwa siku karibu 20 hivi.

 

Maswali / maoni yanakaribishwa.

 

JazakAllah.

 

Visitor's Traces

1,286 Pageviews
Mar. 02nd - Apr. 02nd

Total Page views

762807