Ads 468x60px

Nov 9, 2014

Imam Hussain Radi Allahu Anhu - PT 1 (Kiswahili)
Natumai hamjambo. Kifuatacho ni risala fupi kuhusu kuuawa shahidi kwa mjukuu wa Mtume Swall-Allahu Alaihi Wasallam, Imam Hussein RadwiyAllahu Anhu.
Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi wasallam, aya hapo juu ya 169 kutoka Sura Aali Imran (3), inazungumzia wanaouawa katika njia ya Allah.
 TAFISIRI: Wala usiwadhanie waliouawa katika njia ya Allah kuwa wafu, bali wako hai na wanaruzukiwa kutoka kwa Mola wao Mlezi.
Baada ya Sayyidina Ali kuuawa, mwanae – Imam Hasan, akawa Khalifa wa Waislam. Hata hivyo baada ya miezi kama 6 tu akaachia ngazi na kumuachia ukhalifa sahaba Amirul Muawiya. Siku zake za mwisho zilipofika, alimuita mwanae, Yazid, na kumuusia: baada yangu wewe utashika ukhalifa, ila mshirikishe Imam Husein katika kila jambo, hakikisha kwanza unamlisha na kumnywesha Imam Husein kabla ya kula na kunywa, daima watendee wema Imam Husein, wanafamilia yake na ukoo wa Bani Hashim kwa ujumla. Sisi hatuna haki yoyote katika ukhalifa, ni haki ya Imam Husein, baba yake Sayyidina Ali na watu wa Ahlul Bayt. Utakuwa khalifa kwa muda tu na mara tu Imam Husein atakapokuwa tayari, basi maramoja mkabidhi ukhalifa huo.
Baada ya kifo cha Amirul Muawiya, Yazid akajichukulia madaraka na kutangaza ukhalifa wake. Yazid alikuwa muovu, mwenye tabia mbaya, mwenye kiburi, mlevi, mzinifu, mdanganyifu, mwenye tama, n.k. Hata baadhi ya Masahaba walio hai nyakati hizo walihofia kutelemshiwa kwa adhabu yam awe kutoka kwa Allah kutokana na uovu wa Yazid. Jambo la kwanza alilofanya ni kuwasambaza watu wake sehemu mbalimbali kwa ajili kupata kura ya utii na hasa kina Imam Husein na Masahaba  na tena bila hata ya kuwapa muda wa kuzingatia. Yazid alijua kabisa kuwa ikiwa Imam Husein na Masahaba watampa kura hiyo, basi watu wengine hawatasita kufanya hivyo. Imam Husein naye alifahamu kabisa kuwa ikiwa yeye atampa kura hiyo ya utii mtu muovu kama Yazid, basi ummah wote utamfuata na hivyo muundo mzima wa Uislam utavurugika. Ni kwa sababu hiyo tu Imam Husein alikataa kumuunga mkono Yazid. Hatua hiyo ya Imam Husein ilimuudhi sana Yazid ambaye sasa alianza kumkandamiza na kujaribu kumlazimisha katika suala hilo. Hii ilimlazimisha Imam Husein kuhama mji wa Madina na kwenda Makkah.
Wakati huohuo, Waislam wa Kufa, nchini Iraq, mara kwa mara walimwandikia Imam Husein na kumwomba aende huko ili wao wampe yeye kura ya utii na kuwaongoa na madhalimu ya Yazid. Jumla ya barua kama 150 za kumuomba Imam kwenda huko zilimfikia. Ingawa Imam Husein aliridhia kwenda Kufa kama alivyoombwa, Masahaba walimshauri kuwa makini kwani udanganyifu wa watu Kufa ulikiwa maarufu sana. Imam Husein alisema kuwa sheria inasema kuwa ikiwa Waislam wanakuhitaji uwe kiongozi wao, basi ni jukumu langu la kutikia wito wao la sivyo siku ya Qiyama nitakosa jibu kama nikiulizwa. Hata hivyo, Masahaba walimshauri kuwa ni bora kwanza akamtuma mjumbe wake kwenda kuchunguza hali na ukweli wa wito wao kabla ya yeye kwenda.
Maswali / maoni yanakaribishwa.
JazakAllah,
Muhammad KHATRI

0 comments:

Post a Comment

Enter your Comment here...

 

Visitor's Traces

Total Page views

Follow by Email