Ads 468x60px

Oct 28, 2014

Sayyiduna Umar ibn Khattaab - PT 1‏ (Kiswahili)


Natumai hamjambo. Jana ulikuwa mwezi 26 Mfungo Tatu (Dhul Hijjah) ambamo Khalifa wa 2 wa Kiislam, Sayyidina Umar ibn Khattaab Radwiy-Allahu Anhu, alijeruhiwa vibaya sana akiwa ndani ya sala ya alfajiri. Ifuatayo ni sehemu ya kwanza ya risala.

Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia Rahma Mtume Muhammad Swallallahu Alaihi wasallam, aya hapo juu ya 29 Sura Fatah (48) inazungumzia fadhila za Makhalifa.
TAFSIRI: Muhammad ni Mtume wa Allah, na wale walio pamoja nae ni wakali kwa makafiri ila ni wenye kuhurumiana wao kwa wao, na utawakuta wana rukuu na kusujudu.
Wanazuoni wanasema kwa “walladhina ma-‘ahuu” inammaanisha Sy AbuBakr aliyekuwa pamoja na Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam daima. Kwa “ashiddaahu alal kuffaari” inammaanisha Sy Umar, kwa “ruhamaa-u bainahum” inammaanisha Sy Uthman na “tarahum rukka-an sujjada” inammaanisha Sy Ali. Aya hii inatuelezea kwa mpangilio Ukhalifa wa Makhalifa wanne.
Kusimulia fadhila za Sy Umar kikamilifu katika muda mfupi ni jambo ambalo haiwezekani. Kusilimu kwake, kutangaza dini kwa uwazi, shahada yake, uongozi wake, uadilifu wake, kwa muhtasari tuelewe aliyosema kafiri mmoja kuwa lau kama Waislamu wangekuwa na Umar mwingine, basi leo hii dunia nzima isingekuwa na dhehebu lolote zaidi ya Uislamu.
Makafiri walikerwa mno na uenezaji wa Kiislamu na Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam na hivyo waliitisha kikao Darul Nadwa iliyohudhuriwa na makafiri mashujaa. Kikao iliarifiwa kuwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam amekithiri sana kuwakana miungu yao na hivyo amani kwetu ni kumuua tu (astaghfirullah). Ilipoulizwa nani atakaefanya kazi hiyo? Kwa kuwa Sy Umar alikuwa shujaa sana enzi za ujahili, akakubali kazi hiyo na mara moja alitoka na panga.
Alipoelekea kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasalam, njiani aliulizwa anakoelekea, na alijibu kwenda kumuua Mtume Swallalahu Alaihi Wasallam. Mara moja aliambiwa kwanza aelekee nyumbani kwa dada yake kwani amesilimu pamoja na shemeji wake. Ghadhabu ya Sy Umar ikapanda na mara tu alipofika kwa dada yake, alipiga hodi ya nguvu na mara moja walijua kuwa ni Sy Umar. Sahaba Khubbaab aliyekuwa akitoa taalima, alijificha na Sy Umar alipoingia tu alianza kumpiga dada na shemeji wake hadi kuwajeruhi vibaya sana. Dada yake alimuuliza ewe Umar, je unatupiga kwa sababu tu tumesilimu? Hapo ndipo Sy Umar alitulia na kutaka kuonyeshwa walichokuwa wakisoma. Aliambiwa aoge kwanza na baada ya kusoma aya za Quran, alitaka apelekwe kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam.
Sy Hamza, aliyesimama nje nyumbani kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, alimuona Sy Umar akija na panga na akasema lau kama Umar ana nia mbaya, basi mimi pekee nitamkabili. Sy Umar alipofika kwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam, alisilimu. Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alimuomba Allah siku 2 tu zilizopita kuwa Ainusuru Uislamu kupitia kwa Umar au Abu Jahal. Kipidi hicho Uislamu ulikuwa ukienezwa kwa siri sana, lakini baada ya Sy Umar kusilimu, aliuliza je dini yetu si haki? Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alimuambia bila shaka dini yetu ni ya haki. Hapo ndipo Sy Umar alisema kuwa kuanzia sasa tutaeneza Uislamu kwa kutangaza na si siri tena. Ndipo Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alimpa cheo cha FARUK (mwenye kuleta mfarakano baina ya Uislamu na ukafiri). Hapo ndipo idadi ya Waislamu ilitimia 40. Kusilimu kwa Sy Umar kuliwapa pigo kubwa mno makafiri ambao walisema kuwa leo nguvu yetu imekuwa nusu!!

Maoni / maswali yanakaribishwa
JazakAllah,
Muhammad KHATRI

0 comments:

Post a Comment

Enter your Comment here...

 

Visitor's Traces

Total Page views

Follow by Email